Monday, August 6, 2012

Manji: Yanga inahitaji Sh 570m


MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, jana aliapishwa rasmi kushika nafasi hiyo, sanjari na viongozi wenzake wapya na kufanya kikao cha Kamati ya Utendaji, ambapo baadaye alikiri kuwa klabu hiyo inahitaji shilingi milioni 570 ili kufidia mahitaji ya kujiendesha vizuri.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Manji alisema wamekubaliana kwa pamoja kutafuta vyanzo mbadala vya mapato katika klabu hiyo kukabiliana na pengo la milioni 570 ambalo litaikabili klabu hiyo kwa mwaka na kwa kuanzia wamefikia makubaliano ya kupunguza gharama kwa kufuta posho zote za vikao.

Alisema mbali na hilo pia wamekubaliana kuvunja kamati zote ndogondogo zilizopo ndani ya klabu hiyo kwa lengo za kuziunda upya isipokuwa Kamati ya Uchaguzi pekee ndiyo iliyosalia kutokana na umuhimu wake ndani ya timu.

“Hizi Kamati tunataka ziwe na nguvu na baada ya kuzivunja na kuunda upya tutazipa majukumu yake na kila moja itatakiwa kuanza utekelezaji mara moja na humo ndipo kutajulikana juu ya ujenzi wa uwanja mpya na mambo mengine ya uendeshaji wa timu,” alisema Manji na kuongeza:

“Kamati imekubaliana kuwa taarifa za mapato na matumizi ya klabu zitakuwa zikiandaliwa kila baada ya miezi mitatu na kuwasilishwa katika Baraza la Wadhamini ambao watazipitia taarifa hizo kwa lengo la kujiridhisha, pia mikataba yote ambayo ilishasainiwa itawasilishwa katika baraza hilo na mengine itakayofuata uongozi hautakuwa na uamuzi wa mwisho bali ni Baraza la Wadhamini.

Aidha, Manji alitangaza rasmi kuwa kapteni George Mkuchika ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Rais Utawala Bora, Seif Ahmed na Balozi Ami Mpungwe wamependekezwa na Kamati hiyo ya Utendaji kuingia katika Baraza la Wadhamini huku Mohamed Nyengi na Issack Chanji wakiteuliwa kujaza nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji, ambapo sasa nafasi moja ya mjumbe wa kamati hiyo ikisalia wazi na itajazwa hapo baadaye.

Katika hafla hiyo ya kuapishwa kwa viongozi hao, ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Mama Fatma Karume na mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo Francis Kifukwe, wakati aliyekuwa akiwapisha ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Yanga, Jabir Katundu.

Na Khatimu Naheka,GPL

No comments:

Post a Comment