Mbwana Samatta, juzi aliisaidia timu yake ya TP Mazembe kuiangamiza Zamalek kwenye mchezo wa Klabu Bingwa Afrika na kufufua matumaini ya kutinga hatua ya nusu fainali.
Mazembe ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa Lubumbashi, ushindi ambao unawapa matumaini makubwa Wakongomani hao.
Ushindi huu wa kundi B unawafanya TP Mazembe wafikishe pointi nne wakiwa wamefungana na Berekum ya Ghana wakiwa na pointi mbili nyuma ya vinara Al Ahly ya Misri.
Kipa wa Zamalek, Abdel Wahed Al Sayed, alifanya mambo makubwa baada ya kuokoa michomo kadhaa iliyokuwa inaelekea langoni mwake na kuufanya mchezo huo kufika dakika 70 kwa suluhu.
Lakini dakika chache tangu kipa huyo aokoe mchomo hatari uliokuwa unaelekea langoni mwake, Ngandu Kasongo alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kwanza baada ya kuiwahi krosi safi iliyopigwa kutoka upande wa kushoto.
Samatta ambaye pia alifunga kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Misri mwezi uliopita, aliifungia Mazembe bao la pili katika dakika ya 77 na kuwanyanyua mashabiki 15, 000 waliokuwa wamejazana uwanjani.
No comments:
Post a Comment