Wednesday, June 13, 2012

Kaseja yupo huru kuondoka Simba


KIPA wa Simba, Juma Kaseja (pichani), yupo huru kwa sasa baada ya mwezi huu kumaliza mkataba wake wa miaka miwili aliosaini kuichezea timu hiyo.

Kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo ambacho hakikutaka kutajwa jina, Kaseja amemaliza mkataba wake wa miaka miwili lakini kwa sasa ameanza mazungumzo na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo.

Chanzo hicho kimefafanua kuwa huenda kipa huyo akaongeza miaka miwili mingine ya kuitumikia timu hiyo iliyopo mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam, kutokana na uwezo wake mkubwa na kuwa kiongozi imara ndani ya uwanja.

“Ni kweli Kaseja kamaliza mkataba wake mwezi huu lakini kaanza mazungumzo na mmoja wa watu wanaohusika na suala hilo la usajili, hivyo anaweza akaongeza miaka mingine miwili.

“Kama unavyojua ana uwezo mkubwa na ni kiongozi mzuri uwanjani, nafikiri hiyo ndiyo chachu nyingine inayompa pointi ya kuongeza mkataba,” kilisema chanzo hicho.

Lakini Kaseja hakuwa tayari kukiri kuwa mkataba wake umemalizika. Alizungumza na gazeti hili na kusema: “Mimi natambua ni mchezaji wa Simba na ndiyo maana bado nipo hapa na bado nina mkataba nao.”

Kaseja ambaye ni nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars amekuwa kipa namba moja wa timu hiyo kwa zaidi misimu mitano mfululizo.

Na Lucy Mgina, GPL

No comments:

Post a Comment