Wednesday, June 13, 2012

Straika Amavubi atua Yanga


SIKU chache zimebaki kabla mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Kagame, Mohammed ‘Meddie’ Kagere, hajatua nchini kwa ajili ya kuichezea Yanga.

Kagere, raia wa Rwanda na mshambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Amavubi, amefanikiwa kufanya mazungumzo na Yanga na makubaliano yamefikiwa kwa asilimia 90.

Rafiki wa karibu wa Kagere ambaye ni kati ya makocha waliokuwa wanawania kuifundisha Yanga, ameliambia Championi Jumatano kuwa mshambuliaji huyo hatari, amekubali kutua Jangwani.

Kagere, mwenye uwezo wa kufumua mashuti kwa mguu wa kushoto na kulia, anaichezea Polisi ya Rwanda na alimaliza ligi kuu ya nchi hiyo akiwa wa pili kwa ufungaji wa mabao baada ya kupachika mabao 12, nyuma ya Olviere Karekezi wa APR aliyefunga 14.

Polisi ilifunga jumla ya mabao 37 katika ligi hiyo yenye timu 13.

“Ameniambia kuwa yupo tayari kuja Yanga, alipenda sana kucheza nje ya Rwanda kwa ajili ya changamoto mpya kama nilivyokueleza mimi. Mwaka jana alikuwa ajiunge na St George ya Ethiopia, lakini klabu yake ikakataa.

“Ndiyo maana hakupenda kuongeza mkataba, aliona anaweza kwenda kucheza nje ya Rwanda na sasa Yanga ni chaguo lake. Yanga wamepata mshambuliaji, ana kasi, nguvu na kila wakati ana kiu ya kufunga.

“Nilisikia walimtaka Karekezi, asingekuwa safi kwao. Ingawa anafunga lakini umri wake ni mkubwa na kasi yake imepungua sana, lakini Kagere ni safi zaidi na atawasaidia wakimtumia vizuri,” alisema kocha huyo maarufu ambaye hakutaka kutajwa jina na kuongeza:
“Halafu itakuwa vizuri kwa kuwa Haruna (Niyonzima), anajua namna ya kumchezesha kwa kuwa wamecheza naye timu ya taifa mechi nyingi.”

Upande wa Yanga, mmoja wa wajumbe wanaoshughulikia usajili, alikiri wapo katika hatua nzuri na huenda Kagere akatua nchini ndani ya siku mbili kumaliza kila kitu.
Kagere aliiongoza Polisi kushika nafasi ya pili, APR walikuwa mabingwa kwa pointi 52 wakati Polisi iliboronga baada ya kufungwa mechi mbili za mwisho na kubaki na pointi 50.

Akizungumza jana kutoka jijini Kigali, Rwanda, Kagere alisema yupo tayari kuichezea Yanga.

“Nipo tayari kuichezea Yanga, kikubwa ni suala la makubaliano, sidhani kama haitawezekana. Ila nimewaambia waniache kwa sasa, nataka kuelekeza nguvu zangu kwenye timu ya taifa.

“(Amavubi) tuna mechi ngumu dhidi ya Nigeria wikiendi hii. Nikimaliza, nitakaporejea kutoka huko (Nigeria), tutakaa na kuzungumza na jibu sahihi litapatikana, kama tukimalizana nitakuja, kama ikishindikana nitabaki Rwanda,” alisema Kagere ambaye mwaka jana nusura atue St George ya Ethiopia lakini akashindwa kuelewana ‘lugha’ na uongozi wa Polisi Rwanda.

Kwa mashabiki wa Dar es Salaam, watamkumbuka Kagere wakati wa michuano iliyopita ya Chalenji ambapo Rwanda, Amavubi, chini ya Sredojevich Milutin ‘Micho’ ilishika nafasi ya pili na Kagere akawa mfungaji bora sawa na Karekezi, kila mmoja akiwa na mabao matano.

Kagere alifunga mabao mawili katika mechi ya fainali dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, halafu Rwanda ikashindwa kufurukuta kwenye penalti.

Na Saleh Ally, GPL

No comments:

Post a Comment