Wednesday, April 4, 2012

Kiiza: Julio alinivurumishia mitusi

SIKU chache baada straika wa Yanga, Hamis Kiiza, kunusurika kuzichapa na Kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, mchezaji huyo ameibuka na kudai kocha huyo alimtukana, jambo ambalo lilisababisha apandwe na hasira.

Sekeseke hilo lilitokea Jumamosi iliyopita katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hizo uliopigwa kwenye Dimba la Mkwakwani, Tanga na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Kiiza, raia wa Uganda, ingawa imenyanganywa ushindi huo.

Akizungumza na Championi Jumatano, Kiiza alisema mara baada ya yeye kumfanyia faulo mchezaji wa Coastal karibu na eneo la benchi la timu hiyo, Julio alikuja juu huku akimfokea na baadaye kumtukana jambo ambalo lilimkera.

Alisema baada ya kufunga bao hilo pekee, alikwenda na kuweka kidole chake mdomoni kwa maana ya kumtaka kocha huyo aache kelele.

Kiiza alisema, hajawahi kukorofishana na kocha yeyote tangu aanze kucheza soka lakini kilichotokea katika mchezo huo kilisababishwa na Julio ambaye alishindwa kuonyesha ustaarabu kwa wachezaji, jambo ambalo ni rahisi kuona anavunjiwa heshima yake kama kocha.

“Yeye kama kocha hakupaswa kunifanyia kitendo kama kile, isitoshe huu ni mchezo wa soka, huwezi kujua siku moja tunaweza kukutana katika timu moja, sasa amenitukana kama vile anategemea tutaheshimiana kweli?” alihoji.

GPL

No comments:

Post a Comment