KWELI Waarabu asili yao ni ukorofi! Simba wamejikuta katika wakati mgumu mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene jijini Algiers, Algeria jana mchana na kukutana na vituko vilivyoambatana na vurugu.
Simba imetua jijini humo jana mchana tayari kuivaa ES Setif katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda 2-0 jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba pamoja na viongozi wao walilazimika kusubiri kwa zaidi ya saa mbili uwanjani hapo, huku ubishani na vurugu za hapa na pale zikiendelea.
Maofisa wa uhamiaji nao walishirikiana na viongozi wa ES Setif kuhakikisha wanaiweka Simba katika wakati mgumu baada ya kuzuia vifaa vyao ikiwemo kamera ambayo ilisemekana waliizuia kwa kuhofia inaweza kurekodi mambo yasiyo ya kistaarabu waliyokuwa wakiyafanya.
Akizungumza akiwa uwanjani hapo jana saa 9 alasiri, Rais wa Wanafunzi wa Kiafrika wanaosoma nchini Algeria, Issa Matimbwa, alisema walikuwa kwenye mzozo ambao unaendelea.
“Kama unasikia kuna kelele za kuzozana, kidogo mambo hayajatulia na hawa jamaa si wastaarabu, bado tuko airport. Wanachotaka ni kuwachanganya Simba, ndiyo hivyo tunapigana maana wamezuia vitu kadhaa pamoja na kamera.
“Halafu wanalazimisha waisafirishe timu kwa basi badala ya ndege na sheria za Caf haziruhusu. Rage (pichani) ndiyo anaendelea kupambana nao, sasa nafikiri ungenipa nafasi niendelee kupambana,” alisema Matimbwa na alipoulizwa kuhusiana na wachezaji alisema:
“Wapo hapa ingawa ni mbali kidogo na mimi na wanashuhudia mchezo mzima unavyokwenda ila wameambiwa watulie kabisa na tupo hapa kuhakikisha hakuna mtu yeyote hata kama ni askari anasogea upande huo.”
Juhudi za kumpata Rage kulizungumzia suala hilo zilikwama kwa kuwa alikuwa akipambana kuhakikisha mambo yanakaa sawa.
Kutoka Jiji la Algiers hadi Mji wa Setif ni kilomita 300, wakati Caf hairuhusu timu kusafirishwa kwa basi au treni kwa zaidi ya kilomita 200.
Setif walionyesha nia ya kuzua tafrani mara tu baada ya kuondoka jijini Dar es Salaam baada ya kuandika kwenye mtandao wao kuwa, Simba lazima wasafiri kwa basi au treni.
Matimbwa ambaye ni Mtanzania, anaongoza timu ya wanafunzi wa Kiafrika walio nchini humo kwenda kuishangilia Simba na ataungana na Watanzania wengine wapatao 500 wanaosoma kwenye vyuo mbalimbali nchini humo.
Na Saleh Ally, GPL
No comments:
Post a Comment