Wednesday, May 9, 2012

Mashabiki wa Simba kupiga picha na Kombe Dar Live


BAADA ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa kuifumua Yanga mabao 5-0 kwenye mchezo wa mwisho uliopigwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kikosi kizima cha Simba kinatarajiwa kwenda kufanya sherehe yao kwenye ukumbi wa kisasa wa Dar Live, Mei 27.

Hii inatangazwa kuwa sherehe ya kwanza kubwa ya klabu hapa nchini baada ya kutwaa ubingwa na wachezaji, viongozi, wadau pamoja na mashabiki wa timu hiyo watajumuika pamoja na kupiga picha na kombe lao.

Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga (pichani) aliliambia gazeti hili juzi kuwa sherehe hizo zitakuwa za aina yake, kwa hiyo akawataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kufurahia kwa pamoja ubingwa wao.

“Ubingwa wa mwaka huu umekuwa mtamu sana kwa sababu tumemaliza ligi kwa kishindo baada ya kuwafunga Yanga mabao 5-0 leo (juzi). Kwa hili lazima tujipongeze, kwa hiyo tumeandaa sherehe za kukata na shoka pale Dar Live,” alisema Kamwaga na kuongeza:
“Siku hiyo, tutakuwa na kombe letu ukumbini, mashabiki wetu watapata fursa ya kupiga nalo picha. Viongozi na wachezaji wote wa Simba watakuwepo, kwa hiyo ni nafasi nzuri kwa wanachama na mashabiki kuja kujumuika pamoja.”

Kamwaga aliendelea kusema kuwa sherehe hizo zitaambatana na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wakubwa wa Bongo Fleva na bendi zenye heshima hapa nchini, kwa hiyo akasisitiza kwamba wana-Simba hawatakiwi kukosa.

“Kingine ni kwamba tumeangalia sehemu nzuri ya kufanyia sherehe zetu na tumejiridhisha kuwa Dar Live ndiyo ukumbi muafaka kwa sababu una hadhi ya kimataifa, mandhari yenye hewa safi, yaani unajitosheleza kiburudani,” alisema Kamwaga.

GPL

No comments:

Post a Comment