Wednesday, May 9, 2012

Okwi: Yes nakwenda Azam FC


MSHAMBULIAJI ‘denja’ wa Simba, Emmanuel Okwi (pichani), amesema pamoja na mapenzi yake makubwa kwa timu hiyo lakini yupo tayari kujiunga na Azam.

Okwi, raia wa Uganda, amesema yupo tayari kujiunga na Azam FC ambayo pia itashiriki michuano ya kimataifa baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Azam walianza kumsaka Okwi tangu msimu uliopita lakini juhudi zao zikagonga mwamba ingawa walifanikiwa kumpata beki mwingine kisiki wa zamani wa Simba, Joseph Owino.

Owino na Okwi walitua nchini pamoja na kujiunga na Simba, misimu mitatu iliyopita.

Akizungumza na Championi Jumatano, Okwi alisema hawezi kukataa ofa yoyote itakayopelekwa kwake na Azam, hasa kama ataona ina maslahi kwake na pia kwa Simba.

“Hadi sasa bado sijapata ofa yoyote kutoka Azam wala katika timu yoyote, nimekuwa nikisikia tu kutoka kwenye vyombo vya habari, lakini mimi ni mchezaji, nipo tayari kuondoka Simba iwapo ofa yoyote itakuja kwa maslahi.

“Klabu yoyote ikinifuata kutaka kunisajili msimu ujao itakuwa faida kwangu na kwa Simba kwa jumla.

“Kwa sasa bado nina mkataba na klabu yangu ya Simba, hivyo timu itakayonihitaji ni lazima ivunje mkataba kulingana na makubaliano,” alisema Okwi.

Tayari Azam FC ilishaanza mazungumzo kimya kimya na Simba, mara ya mwisho ‘Lambalamba’ waliahidi kutoa kitita cha Sh milioni 50 pamoja na Mrisho Ngassa ili wapewe Okwi.

Lakini taarifa zinaeleza kuwa, uongozi wa Simba ‘ulitoa nje’ ingawa nao ulikuwa ukiwabembeleza Azam FC umpate Ngassa kwa kuwa alikuwa pendekezo la Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic.

Milovan anataka kumtumia Ngassa kama kiungo mshambuliaji wa kulia na Okwi kushoto huku Haruna Moshi ‘Boban’ akigonga namba ‘ten’ na Sunzu anamaliza kati, yaani tisa.

Na Khadija Mngwai, GPL

No comments:

Post a Comment