Monday, August 6, 2012

TP Mazembe kupima wachezaji wapya Simba


SIMBA inatarajia kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, APR ya Rwanda au Azam FC katikati ya mwezi huu, kwa lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya familia ya marehemu Patrick Mutesa Mafisango.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alisema tayari utaratibu wa kuileta timu mojawapo kati ya hizo umeshakamilika.

Alisema fedha zitakazopatikana kwenye mechi hiyo, zitatunisha mfuko wa zile ambazo familia ya Mafisango itapewa.

“Tumeshafanya mazungumzo na klabu ya TP Mazembe, APR ya Rwanda na Azam FC, klabu ambazo Mafisango aliwahi kuzichezea. Tunataka kucheza mechi moja ya kirafiki, maalum kwa ajili ya kukusanya fedha tutakazozitoa kwa familia yake.

“Tunatambua hali halisi ya mazingira ya familia ya Mafisango ilivyo, ni kweli inahitaji msaada wa hali ya juu, hivyo, sisi kama Simba tunaliangalia hilo na tayari tumeshafikia makubaliano na klabu hizo, mojawapo itakuja kwa lengo la kucheza mechi hiyo ambayo ni muhimu,” alisema Kaburu.

Alisema watajipanga kuhakikisha fedha zote zitakazopatikana kwenye mechi hiyo, zinakuwa ni mchango kwa familia ya mchezaji huyo na si vinginevyo, kwa lengo la kuhakikisha watoto wake wanapata haki yao.

Na Khadija Mngwai, GPL

No comments:

Post a Comment