Saturday, July 21, 2012

ZIFF 2012: Filamu za Kiswahili zavunja rekodi


TAMASHA la 'Zanzibar International Film Festival' la 15 limemalizika jumapili iliyopita ambalo kwa mwaka huu limeonyesha filamu zaidi ya 105 kutoka nchi 35 zilizowakilisha mabara yote.

Nigeria, Kenya, Uganda, Italy, Marekani, Iran, Sudan, Afrika Kusini, Rwanda, Ufaransa, Mexico ni baadhi tu ya nchi zilizoshiriki katika tamasha la mwaka huu.

Mbali na kuonyesha filamu pia tamasha liliandaa warsha mbalimbali maalumu kwa watu wanaojihusisha na utengenezaji wa filamu kuondoka na elimu mpya.

Wataalam wa kamera na uongozaji wa filamu Nicolas Staple, Barry Braverman na Mario Van Peebles waliongoza warsha hizo.

Tunzo
Miaka yote tamasha hutoa tunzo kwa filamu na washiriki wa tamasha, mwaka huu kulikuwa na tunzo nyingine za Zuku, Verona, Ousmane Sembene na Signis.

ZIFF ilitoa tunzo saba ikiwemo na filamu bora, mwigizaji bora wakati Zuku ilitoa tunzo tatu kwa Filamu Bora ya Kiafrika na Waigizaji Bora wa Kike na wa Kiume.

Filamu za Chungu na Zamora ziliweka historia kwa kutwaa tunzo katika usiku huo.Mara nyingi filamu zinazoshinda huwa huenda zimetengenezwa na Watanzania walio nje ya nchi au imeongozwa na mtu kutoka nje ya nchi.

Chungu na Zamora ni filamu zilizotengezwa na na zimechezwa, zimeongozwa na Watanzania.

Zuku na filamu za Kiswahili
Mdhamini mkuu wa tamasha hilo, Kampuni ya Ving'amuzi, Zuku imeanzisha channeli ambayo itakuwa ikionyesha filamu za Kiswahili tu.

Mwenyekiti wa Wananchi Group inayomiliki Zuku, Ali Mufuruki amesema kampuni hiyo imefungua mwanya mwingine wa kuwawezesha watengenezaji wa filamu nchini.

"Zuku itakuwa na jukumu muhimu katika kupandisha viwango vya ubora wa filamu za Kiafrika kwa sababu inatoa nafasi kwa watengenezaji wa filamu na wazalishaji kuuza na kuonyesha bidhaa zao. Aidha, Zuku hasa ina nia ya kukuuza vipaji vya ndani na kutangaza kazi zao,alisema na kuongeza.

"Tumeidhamini ZIFF kwa miaka kumi, lengo letu ni kupata kazi zenye ubora kwa kuwa tunataka kuona tasnia hii inakuwa katika ukanda huu wa Afrika," anasema Mufuruki.

Mwelekeo wa ZIFF
Afisa Mtendaji Mkuu wa ZIFF, Ikaweba Bunting amesema mwelekeo wa tamasha hilo ni kuikuza tasnia ya filamu barani Afrika ingawa anakiri kuwa changamoto bado ni nyingi.

"Kwa miaka 15 ZIFF imejitahidi kuinua sanaa hii, ingawa njia haikuwa tambarare lakini tumejitahidi kufika hapa na matunda kila mmoja wetu anayaona," anasema na kuongeza.

"Lengo letu ni kufanya mambo makubwa zaidi ambayo mengi huwa yanakwamba kutokana na kukosa ufadhili wa kutosheleza kila kitu, bado tunahitaji kusaidia katika kulisukuma hili gurudumu la kuobadilisha sekta ya filamu Afrika," anasem Bunting.

Julieth Kulangwa, Aliyekuwa Zanzibar

No comments:

Post a Comment