Friday, July 6, 2012

TAARIFA KUTOKA TFF LEO JULAI 6, 2012


Release No. 109
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Julai 6, 2012

16 BORA COPA COCA-COLA KUANZA J’MOSI
16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 inaanza kesho (Julai 7 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazokutanisha timu nane kati ya 16 zilizofuzu hatua hiyo. Mechi hizo za 16 bora zitachezwa kwenye viwanja vya Kumbukumbu ya Karume na Tanganyika Packers vya Dar es Salaam.

Ruvuma iliyoongoza kundi A itacheza na Temeke iliyoshika nafasi ya tatu kundi C. Mechi hiyo itaanza saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Karume. Mechi nyingine ya asubuhi itakayochezwa Tanganyika Packers itawakutanisha washindi wa pili kundi A Kigoma dhidi ya Mara walioshika nafasi ya nne kundi C.

Mechi za jioni kwa kesho zitakazoanza saa 10 kamili jioni zitakuwa kati ya Mjini Magharibi na Kagera kwenye Uwanja wa Karume wakati Morogoro na Pwani zitaumana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.

Hatua ya 16 bora itakamilika keshokutwa (Julai 8 mwaka huu) kwa mechi za asubuhi kati ya Kinondoni na Rukwa kwenye Uwanja wa Karume, na Dodoma dhidi ya Arusha kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers. Mechi za jioni siku hiyo ni kati ya Kilimanjaro na Mwanza (Uwanja wa Karume) na Tabora na Tanga (Tanganyika Packers).

Timu zitakazoshinda zitaingia hatua ya robo fainali itakayochezwa Julai 10 na 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Nusu fainali itachezwa Julai 13 mwaka huu, na kufuatiwa na mechi ya mshindi wa watatu na fainali ambazo zote zitachezwa Julai 15 mwaka huu.
SABA WAPATA ITC KUCHEZA KENYA, MSUMBIJI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania saba kucheza mpira wa miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji.

TFF imetoa hati hizo kwa wachezaji hao baada ya kuombewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Msumbiji (FMF) ili waweze kucheza katika klabu za nchi hizo.

Wachezaji waliokwenda Bandari ya Kenya na klabu walizokuwa wakichezea nchini kwenye mabano ni David Naftali (huru), Meshack Abel (huru), Mohamed Banka (huru) na Thomas Mourice (Mtibwa Sugar).

Klabu ya CD Madchegde ya Msumbiji imewachukua wachezaji Hassan Hassan Mustapha kutoka Mgambo Shooting ya Tanga, na Abdallah Ally Abdallah na Thobias David Silas kutoka klabu ya daraja la kwanza ya Transit Camp ya Dar es Salaam.

ODHIAMBO WA AZAM APATA ITC
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji George Odhiambo, raia wa Kenya aliyejiunga na klabu ya Azam.

Hati hiyo imetolewa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU) ambapo Odhiambo alikuwa akicheza nchini humo kabla ya kutua Azam kwa ajili ya msimu wa 2012/2013.

Klabu nyingine zinazosajili wachezaji kutoka nje ya Tanzania zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha uhamisho wao (transfer) kabla ya Julai 30 mwaka huu ambayo ndiyo siku ya mwisho kufanya hivyo.

Kanuni ya 41 ya Ligi Kuu kuhusu ITC inasema: “(1) Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wa kulipwa yatawasilishwa kupitia mtandao wa kompyuta kwa kutumia program ya ‘Transfer Matching System-TMS’ baada ya klabu zinazohusika na mchezaji huyo au wachezaji hao kukubaliana nje ya mtandao.

(2) Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wasio wa kulipwa yatawasilishwa kwa barua TFF baada ya klabu zinazohusika na mchezaji huyo au wachezaji hao kukubaliana. Chama cha Soka kinachotoa ITC kwa njia hii kitapeleka nakala FIFA. (3) ITC haihitajiki kwa mchezaji mwenye umri chini ya miaka kumi na mbili (12).”

Tunapenda kuzikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 53 ya Ligi Kuu, wachezaji wa kigeni ni lazima wawe wanachezea timu ya Taifa au klabu za Ligi Kuu huko wanakotoka.

Kanuni hiyo inasema: “Klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wa ngazi ya kimataifa ambao ni wa timu za Taifa na Ligi Kuu kutoka nje ya nchi wasiozidi watano (5). Wachezaji kutoka Ulaya na Marekani ya Kusini wanweza kuwa wa daraja la pili na kuendelea, na klabu inaruhusiwa kuchezesha wachezaji walioorodheshwa wasiozidi watano (5) wa kigeni katika mchezo mmoja. Wachezaji hao watasajiliwa baada ya TFF kuhakikisha usahihi wa taarifa zao na kukamilika kwa taratibu za uhamisho wa kimataifa.”

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment