Thursday, June 21, 2012

Simba bila Okwi Kagame Cup


WAKATI patashika la michuno ya Kombe la Kagame 'ikinukia', mabingwa wa soka nchini, Simba ya jijini Dar es Salaam itamkosa mshambuliaji wake wa kimataifa toka Uganda, Emmanuel Okwi.

Okwi ataikosa michunao hiyo ya wiki mbili itakayofanyika mwezi ujao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa sababu atakuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Nyota huyo mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2011/2012 kwa wale wa nje wanaocheza soka nchini, anakwenda kujiunga kwa muda na klabu ya Orlando Pirates.

Okwi ambaye kwa sasa yuko Uganda alikokwenda kuicheza timu ya taifa kwenye michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, hatarejea nchini bali ataunganisha moja kwa moja Afrika Kusini.

Akizungumza na Mwananchi, kiongozi mmoja wa Simba bila kutaka jina lake kuandikwa, alisema Okwi anatarajia kuondoka wiki ijayo na ataikosa michuano ya Kombe la Kagame.

"Kuna mambo machache tunamalizia pamoja na klabu anayokwenda kucheza, tunatarajia mpaka kufikia Jumapili tutakua na jibu la uhakika kuhusu hatima yake kipindi hiki cha majaribio yake," alisema mtoa habari.

Kuhusu kurudi kwa Kocha Mkuu, Curkoviv Milovan, alisema anatarajia kurudi nchini Jumapili wiki hii, huku Felix Sunzu naye akitarajia kuwasili Jumatatu ijayo.

Michuano ya Kombe la Kagame inatarajia kuanza Julai 14, ambapo Tanzania itawakilishwa na mabingwa watetezi, Yanga, Simba na Azam FC.

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kinataraji kuondoa kesho kuelekea Mikoa ya Kanda ya Ziwa kucheza mechi chache za kirafiki.

Jessca Nangawe, Mwananchi

No comments:

Post a Comment