Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
****
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema mapinduzi ya uongozi yaliyofanywa na wanachama wa klabu ya Yanga ni batili na yako nje ya mstari halali wa katiba ya klabu hiyo, hivyo hawatakuwa tayari kuyatambua.
Kauli ya kutoyatambua mapinduzi hayo, pia imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Jaji John Mkwawa aliyewataka wanachama walioitisha mkutano huo kwenda kusoma upya katiba ya klabu hiyo.
Jumapili iliyopita, wanachama 721 walikusanyika makao Makuu ya Klabu hiyo mtaa wa Jangwani na kuung'oa madarakani uongozi wao chini ya Mwenyekiti Lloyd Nchunga.
Kungolewa kwa uongozi huo kulikuja baada ya wiki kadhaa kuwapo na shinikizo la kuutaka kuachia ngazi kwa madai ya kushindwa kuongoza klabu kwa mafanikio ikiwa pamoja na kutoitisha Mkutano Mkuu muda mrefu.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kilichofanywa na wanachama hao dhidi ya uongozi wao ni kinyume na katiba ya TFF na vilevile kinyume na katiba klabu hiyo.
Osiah alisema TFF iko tayari kutambua mabadiliko ya uongozi kwenye klabu, lakini ni yale tu yatakayofuata taratibu za kikatiba na siyo kinyume chake kama walivyofanya wanachana wa Yanga.
Kwa maana hiyo, TFF haitakuwa tayari kufanya kazi na viongozi wa muda watakaowekwa madarakani na wanachama wa Yanga, alisema zaidi Osiah huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu katiba.
"Tunafahamu na kufuatilia kwa karibu yanayotokea Yanga, lakini ni lazima pia tutoe tahadhari kwa wananchama kuwa makini na uamuzi watakaotoa," alisema.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkwawa alisema walichofanya wanachama hao ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba kwani hakuna kifungu kwenye katiba ya Yanga kinachoruhusu mapinduzi ya uongozi.
"Katiba ya Yanga na ile ya TFF haikubali kuondoa uongozi kwa nguvu ya umma, walichofanya wamekiuka katiba yao, ya TFF, Cecafa, Caf na Fifa, "alisema Jaji Mkwawa.
"Namshauri Nchunga, kwa vile kuna wajumbe wa kuchaguliwa wamejiuzulu basi aitishe haraka Mkutano Mkuu wa dharura waandae uchaguzi mdogo ili kuziba nafasi za waliojiuzulu," alisema.
Alisema kamati ya utendaji ya Yanga inaundwa na wajumbe nane wa kuchaguliwa na watatu wa kuteuliwa na mpaka sasa wajumbe wakuchaguliwa walioachia ngazi ni Mbaraka Igangula, Mzee Yusuf, Pascal Kihanga, Davis Mosha, Seif Mohamed, Ali Mayay na Mohamed Bhinda ambaye pamoja na awali kusema angejiuzulu bado hajafanya hivyo mpaka sasa.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga ibara ya 22 (2) inayozungumzia mkutano wa dharura inasema: "Endapo nusu ya wajumbe (wanachama) wamewasilisha ombi kwa Kamati ya Utendaji kwa maandishi, kamati italazimika kuitisha mkutano kwa kipindi kisichozidi siku 30 baada ya ombi hilo kuwasilishwa.
Kipengele cha (3), wito wa mkutano unatakiwa utolewe angalau siku 15 kabla ya mkutano wakati kipengele cha (4) kinasema ajenda, nyaraka muhimu zipelekwe kwa wanachama siku saba kabla ya mkutano.
Mwananchi ilipomtafuta Katibu wa Baraza la Wazee Ibrahim Akilimali hakuweza kupatikana, wakati Mwenyekiti wa kikao Bakili Makele akikataa kuzungumza kwa undani suala hilo zaidi ya kusema kuwa walikuwa bado kuwasilisha taarifa ya kikao chao, TFF na Msajili wa Vilabu.
Katibu mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa alisema: "Kikao cha Kamati ya Utendaji kinakaa wakati wowote kuanzia sasa, lakini kwa sasa ziwezi kuzungumza lolote kwa kile kinachoendelea Yanga."
Hata hivyo Nchunga hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo kwani awali simu yake iliita bila majibu na baada ya muda mfupi hakupatikana kabisa hewani.
Sweetbert Lukonge, Mwananchi
No comments:
Post a Comment