KINARA wa kuzifumania nyavu msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika hivi karibuni, John Boko amesema hafikirii na wala hana mpango wa kuhama Azam FC na kujiunga na timu nyingine nchini.
Hivi karibuni kulikuwa na taarifa kwamba nyota huyo wa Azam alikuwa na mpango wa kuhama na kujiunga na moja ya vigogo vya soka nchini, aidha Simba au Yanga
Akiongea na Mwananchi, Boko alisema hajawahi kuwa na wazo la kutaka kuhama Azam aliyoiwezesha kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya pili kwa mara ya kwanza msimu huu.
Lakini amesema, kama ataona ipo sababu ya kuhama Azam basi lengo lake ni kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
Akizungumza jana, Boko alisema pamoja na mkataba wake kufikia tamati, lengo lake bado ni kuendelea kuicheza Azam.
"Simba na Yanga haziko kwenye mpango wangu, nafikiria zaidi kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Nakata kujitangaza," alisema Boko.
"Kipindi hiki cha usajili kila timu inataka kuongeza nguvu, lakini kwa upande wangu bado naamini nitabaki Azam," alisema.
Boko aliyemaliza msimu kwa kupachika wavuni mabao 18, alisema lengo lake ni kuisadia Azam katika michuano ya kimataifa wanayochezwa kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Wakati huohuo, mshambuliaji wa Villa Squad iliyoshuka daraja, Nsa Job yuko kwenye hatua za mwisho kusaini mkataba wa kujiunga na Coastal Union ya Tanga.
Awali Nsa aliyezichezea klabu za Yanga, Azam, Moro United na Villa Squad za jijini Dar es Salaam alidai anahitaji Sh20 milioni na mshahara wa Sh2 milioni kwa mwezi ili aweze kumwaga wino wa kujiunga na mabingwa hao wa ligi mwaka 1988.
Nahodha huyo wa Villa aliliambia Mwananchi jana jijini Dar es Salaam: "Tumefika kwenye hatua nzuri ya makubaliano ya kusaini mkataba na Coastal." Nsa aliyeweka rekodi nzuri ya kupachika bao kila mechi kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
"Siwezi kuweka wazi ni kiasi gani cha fedha tulichokubaliana na Coastal, ni siri yangu na uongozi huo." alisema Nsa aliyefunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu iliyofika kikomo Mei 6, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora alisema: "Ni kweli Nsa ni chaguo letu la kwanza, tumemfuatilia kwa ukaribu sana na kubaini ni aina ya mchezaji tunayemuhitaji kwenye kikosi chetu."
Jessca Nangawe na Calvin Kiwia
No comments:
Post a Comment