Tuesday, April 17, 2012

Simba SC kubwa kuliko


SIMBA imefanikiwa kujikita kileleni kwa tofauti ya pointi tatu baada ya jana kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kiungo raia wa Rwanda, Patrick Mafisango, ndiye aliyekuwa shujaa wa Simba katika mchezo huo uliokuwa mgumu baada ya kufunga bao pekee katika dakika ya 81 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Emmanuel Okwi.
Simba walijitahidi kutafuta bao dakika 80 za mchezo bila mafanikio huku wachezaji wake, Gervais Kago, Salum Machaku, Haruna Moshi ‘Boban’ na Patrick Mafisango wakikosa mabao ya wazi kwa nyakati tofauti.
Mafisango alikosa bao la wazi katika dakika ya 78 baada ya kupiga shuti lililokwenda juu ya lango akipokea pasi ya Amir Maftah, lakini dakika tatu baadaye akasawazisha makosa kwa kufunga bao hilo pekee.
Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa Simba kupata ushindi huo kwani maafande wa Ruvu Shooting walilisakama lango la wapinzani wao mara kadhaa, lakini wakakosa umakini katika umaliziaji.

Katika dakika ya 17, mpira mrefu uliopigwa na Hassan Dilunga wa Ruvu uliwakuta kiungo mkongwe, Mohammed Kijuso na Rafael Keyala lakini wakategeana kupiga na kumpa nafasi beki, Victor Costa kuuokoa.

Kwenye mchezo huo, mpira ulisimama kwa sekunde kumi kutokana na Simba kuzidi kwenye benchi la ufundi, walikuwa 12 ndipo mwamuzi Rashid Msangi kutoka Singida akaamuru mmoja apungue na kinda Kessy Rajab akaondolewa.

Dakika ya 30, Victor Costa, akiwa kwenye eneo la hatari, alipokea pasi ya Boban iliyotokana na mpira mrefu wa faulo iliyopigwa na Machaku lakini akapiga shuti hafifu lililopaa nje ya lango.

Ruvu wangeweza kupata bao katika dakika ya 46 wakati Abdallah Juma akiwa yeye na mlinda mlango, Juma Kaseja, alipopiga mpira uliotoka nje ya lango.

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Milovan cirkovic, alisema: Nimefurahishwa kuona timu imeshinda lakini sijafurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu, nadhani kimetokana na uchovu, tangu tutoke Algeria hatujafanya mazoezi magumu, lakini nimejua makosa na nitayafanyia kazi.”

Naye Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa, alisema ameyapokea matokeo ingawa alikiri kuwa, safu zake za ushambuliaji na ulinzi zimemuangusha kutokana na kutokuwa makini.

Wakati huohuo, kipa wa Simba, Juma Kaseja aliingia uwanjani hapo akiwa amevaa tisheti yenye maandishi ya kukumbuka kifo cha aliyekuwa mchezo filamu mahiri hapa nchini Steven Kanumba, ambaye amefariki wiki moja iliyopita.


Na Khatimu Naheka, GPL

No comments:

Post a Comment