Tuesday, April 17, 2012

MSANII WA BONGO FLEVA MATATANI KIFO CHA KANUMBA


STAA wa muziki wa Bongo Fleva hapa nchini, ameingia matatani baada ya kudakwa na polisi na kuhojiwa kwa saa kadhaa kwa madai kuwa ndiye aliyemtorosha msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’, usiku baada ya kugundua kuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba amefariki dunia.

Chanzo chetu cha habari ndani ya jeshi la polisi kinadai kuwa msanii huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama), alikamatwa siku chache baada ya maziko ya Kanumba kumalizika, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kiliongeza kuwa ni kweli msanii huyo alikamatwa ili kuisaidia polisi kwani ilidaiwa alikwenda kumchukua Lulu eneo la tukio na kumpeleka kusikojulikana.

Aidha, chanzo hicho kilisema kesi hiyo sasa imehamishwa kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay na sasa inashughulikiwa na maofisa upelelezi wa kituo cha kati ambako mahojiano hayo yalifanywa kwa siri kubwa ili kulinda usalama wa msanii huyo.

“Baada ya kumhoji msanii huyo na kupata kile walichokuwa wanakitaka, walimuachia bila masharti yoyote lakini aliambiwa akihitajika tena watamwambia,” kilisema chanzo hicho.

Aidha, waandishi wetu walipofuatilia sehemu mbalimbali kutaka kujiridhisha kuhusiana na tukio hilo, inadaiwa kuwa siku ya kifo cha Kanumba, mwanamuziki huyo alipigiwa simu na Lulu aliyetaka aende kumtoa eneo la tukio.

Gazeti hili lilimhoji mwanamuziki huyo na alipoulizwa kuhusu kukamatwa, aliruka na kusema hajakamatwa na yupo huru akiendelea na shughuli zake kama kawaida.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela, alipohojiwa kuhusiana na kudakwa kwa msanii huyo, alisema si vyema kusema kuwa wamemkamata msanii yeyote kuhusiana na tukio hilo kwani kwa kufanya hivyo watahatarisha maisha ya mhusika.

“Katika mfumo wa kiuchunguzi si vyema kusema chochote kuhusiana na upepelezi wetu kwani kazi bado tunayo, hata kama ingekuwa kweli bado tusingezungumza lolote, hizo ndizo kanuni zetu,” alisema Kamanda Kenyela.


Makongoro Oging na Haruni Sanchawa

No comments:

Post a Comment