Wednesday, February 8, 2012

Vengu alicheleweshwa India - Dokta


MMOJA wa madaktari wanaomtibu msanii ‘jembe’ wa Kundi la Orijino Komedi, Joseph Shamba ‘Vengu’ (pichani) nchini India ameeleza kuwa, kutokana na ugonjwa unaomsumbua alitakiwa awahishwe kwa matibabu lakini amecheleweshwa.

Mmoja wa Wabongo anayeishi nchini humo aliyejitambulisha kwa jina la Muddy alisema, hivi karibuni alimtembelea Vengu katika Hopitali ya Apoll Hospital Hydevabad na kubahatika kuzungumza na mmoja wa madaktari wanaomtibu.

“Nilikwenda pale hospitali kumjulia hali Albert Makoye (Mkuu wa Itifaki na Nidhamu wa Miss Tanzania) aliyekuwa anapata matibabu.

“Baada ya hapo nilikwenda pia kumuona Vengu, alikuwa akitibiwa pale lakini niliongea na mmoja wa madaktari ambaye aliniambia kuwa, wanajitahidi kumtibu na wanaamini atapona ila amechelweshwa kupelekwa,” alisema mtoa habari huyo.

Akizungumza na mwandishi wetu Makoye alikiri kutembelewa na Muddy na kueleza kuwa, hata yeye alipata fursa ya kwenda kumjulia hali Vengu.

“Muddy alinitembelea pale hospitalini nilipokwenda kwa matibabu na hata mimi nilipopata nafuu nilikwenda kumuona kwani tulilazwa hospitali moja, madaktari wanapambana kumrudisha Vengu katika hali yake ya kawaida,” alisema Makoye.

Vengu amekuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi yanayoshambulia seli za mfumo wa fahamu kichwani ambayo kitaalamu yanaitwa Brain au Cerebral Atrophy na kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu.

Habari na GPL

No comments:

Post a Comment