Thursday, February 2, 2012

Mgomo wa Madaktari, Manyaunyau chereko


WAKATI madaktari wa hospitali za serikali nchini wameweka ngumu kutibu wagonjwa wakidai kuboreshewa mishahara, baadhi ya waganga wa kienyeji wameonekana kufurahia kwa sababu sasa wanapata wagonjwa wengi wanaotaka tiba kwao.

Uchunguzi wa Amani uliofanywa Jumapili iliyopita ulibaini kuwa, baadhi ya waganga hao wamekuwa wakiongeza kipato kila kukicha tangu hali ya tiba kwenye hospitali hizo ilipokuwa mbaya.

Mganga wa kienyeji, Jongo Salum ‘Manyanyau’ (pichani) wa jijini Dar, alithibitisha kupokea wagonjwa wengi ambao ndugu zao wamewahamisha kutoka katika hospitali mbalimbali za serikali, Dar.

“Ni kweli huu mgomo wa madaktari umetunufaisha sana sisi waganga wa jadi, siku hizi tunapokea wagonjwa wengi kuliko zamani, hata mifuko yetu imetuna,” alisema Manyaunyau.

Msafiri Pesambili ‘Wakunyumba’ yeye ni mtaalamu wa tiba za asili Magomeni-Kagera, Dar, alisema tangu mgomo wa madaktari uanze, anapata wagonjwa kuanzia 15 hadi 20 kwa siku, wengi wao wakitokea Muhimbili.

“Siwezi kusema madaktari waendelee kugoma ili nipate wagonjwa wengi, ila ukweli ni huo kwamba kwa siku mbili tatu hizi, kidogo Mungu ametuona.

“Siku hizi napata wagonjwa kuanzia kumi na tano hadi ishirini kwa siku,” alisema Wakunyumba.

Bi Hawa Mfaume wa Kliniki ya Mwangaza, Temeke, Dar alisema amekuwa akipokea wagonjwa wengi ambao ndugu zao wamewapeleka kutoka kwenye hospitali zenye mgomo.

Habari tulizozipata wakati tunakwenda mitamboni zilidai kuwa, hali ndani ya wadi katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili ilikuwa imezidi kuwa mbaya baada ya wagonjwa wengi kufia humo bila kupatikana madaktari wa kuidhinisha vifo vyao ili maiti ziondolewe.

Na Issa Mnally, GlobalPublishers

No comments:

Post a Comment