Tuesday, September 20, 2011

Waliokufa katika ajali ya MV Spice Islander ni 1741; Mbunge atoa idadi ya waliofariki kila Mkoa wa Pemba

Mbunge wa Jimbo la Ziwani, mkoani Pemba kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Ahmed Juma Ngwali amedai kuwa takwimu zilizotolewa na wakuu wa wilaya kwa Makamu wa kwanza wa Rais Maalim Hamad zimetofautiana kidogo, kwani idadi ya waliokufa katika ajali ya meli ya MV Spice Islander ni 1,741.

Ngwali anasema alifanya utafiti kwa kuzungukia maeneo walikotoka waliokufa kwa kutumia usafiri wake mwenyewe na kwa msaada wa watu waliopoteza ndugu zao, ambapo baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alifanya ziara Kisiwani Pemba kuwafariji wafiwa na kuwapa pole waliopotelewa na ndugu zao, na kubaini idadi hiyo kubwa.

Akazitaja takwimu za waliokufa katika ajali hiyo kwa kila mkoa Kisiwani Pemba kuwa ni kama ifuatavyo:
Koani watu 27 (na siyo 24 waliotajwa)
Chakechake watu 146
Micheweni 367
Wete 1,204
"Mfano kwenye Jimbo langu la Ziwani watu waliopoteza maisha ni 84, ambapo wanawake ni 44 na wanaume 40, katika idadi hiyo watoto wenye umri kati ya miaka 16 ni 50, vichanga na mwanaume aliyefahamika kama Lujaima Omar Suleiman wa Kijiji cha Kwale, aliyepotea pamoja na mama yake", anasema Bw. Ngwali.

Alisema katika mchanganuo huo, Jimbo la Ziwani hususan Kijiji cha Ziwani ndicho chenye idadi kubwa ya waathirika wa meli hiyo, baada ya kupoteza watu 46, huku Kijiji cha Nyiapi kikiwa na idadi ndogo ya watoto wawili Khamis Ali Faki na Juma Kombo Hamad.

Ngwali alibainisha kuwa meli hiyo ilikuwa na abiria zaidi ya 2,360, idadi ambayo ni kikubwa kuliko uwezo wa meli hiyo na kuonesha kuwa na uhakika na maelezo yake, aliahidi kuwa iwapo itathibitika kasema uongo kuhusu idadi hiyo ya waliokufa katika ajali, yuko tayari kuachia ngazi, "Ninachosema ndio ukweli ya jambo hili ulivyo, kama itabainika kuwa nimesema uongo, niko tayari kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Ziwani, waliokufa ni wengi tofauti na idadi inayotajwa na serikali ya Zanzibar", anasema Bw. Ngwali.

Ngwali alisema idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na idadi aliyotaja kuwa ya mikoa ya Pemba, ambayo haikuhusisha wakazi wa Unguja.

Alisema katika suala kama hilo la vifo vya wananchi siasa haina nafasi, hivyo ameitaka Serikali kusema ukweli kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha na 619 waliookolewa.

[sehemu hii ya taarifa imenukuliwa kutoka gazeti Majira, imeandikwa na Nyakasagani Masenza]


Na Wavuti.Com

No comments:

Post a Comment