KOCHA Mkuu wa TP Mazembe, Lamine ND’iaye amemuonya mshambuliaji wake kinda, Mbwana Samatta kuhakikisha anazitumia nafasi za kufunga mabao anazozipata.
ND’iaye raia wa Senegal, amemtaka Mbwana na washambuliaji wengine wa timu hiyo kufunga mabao kila wanapopata nafasi ili kuipa uhakika wa ushindi timu hiyo.
Kocha huyo ameuambia mtandao wa klabu hiyo maarufu barani Afrika kuwa hakufurahishwa na Mbwana na washambuliaji wengine wa timu hiyo katika mechi yao ya Ligi Kuu ya DR Congo ‘Lina Foot’ dhidi ya Elima waliyoshinda kwa mabaoi 5-2, mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Tungeshinda hadi mabao 10, kingekuwa ni kitu kizuri zaidi lakini nafasi nyingi za uhakika tumepoteza. Mputu, Samatta na Singuluma hawakuwa makini. Ni vizuri kutumia nafasi na kupata mabao mengi zaidi,” alisema ND’iaye.
Pamoja na upinzani mkubwa wa namba kutoka kwa washambuliaji nyota wa TP Mazembe, ND’iaye amemuamini Samatta kwa kumpa nafasi ya kucheza katika mechi nyingi muhimu za timu hiyo.
Samatta alijiunga na Mazembe akitokea Simba na amekuwa kati ya wachezaji waliowashangaza Wakongo kutokana na kupata namba mapema katika kikosi hicho bila ya kujali ugeni wala umri wake.
TP Mazembe ambayo hivi karibuni ilinunua ndege mpya iko katika mikakati ya kurejesha heshima yake ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Na Global Publishers Tz
No comments:
Post a Comment