Friday, August 5, 2011

Mgosi: Motema Pembe zaidi ya Simba


Na Khadija Mngwai
MSHAMBULIAJI Mussa Mgosi (pichani) amesema klabu yake mpya DC Motema Pembe ya DR Congo ni zaidi ya Simba kutokana na programu za timu hiyo pamoja na mfumo wa uendeshaji wa klabu kutokuwa na wanachama na badala yake kuwa na wapenzi tu.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mgosi alisema Motema Pembe haina wanachama kama ilivyo Simba, hivyo kufanya uamuzi kutolewa na Rais wa klabu, Mussa Nganya, jambo linalofanikisha kutokuwepo kwa mikwaruzano ya hapa na pale.

“Motema Pembe ina utofauti mkubwa na klabu ya Simba kutokana na kutokuwa na wanachama kama ilivyo kwetu, timu ina wapenzi tu na uamuzi wote unatolewa na Rais Mussa Nganya na hakuna mizengwe yoyote, hivyo kufanya kila kitu kiende sawa.

“Mfumo wa soka la Congo ni mzuri kutokana na programu wanazotumia katika ligi kuchangia wachezaji wawe na viwango bora kulinganisha na kwetu. Nimefurahishwa na mfumo wa wachezaji wa Congo kwani wote malengo yao kwenda nje tu na siyo kuishia hapa, hii inanipa changamoto ya kusonga mbele zaidi ya kujituma,” alisema Mgosi.

Pia, aliwataka wachezaji waliocheza muda mrefu Simba na Yanga kuangalia uwezekano wa kuachana na timu hizo kwa kuwa yatawafika kama yaliyomtokea yeye. Mgosi alitemwa katika usajili uliofungwa hivi karibuni kwa kile kilichoelezwa kuwa kiwango chake kimeshuka.

No comments:

Post a Comment