Monday, August 22, 2011

MASENGENYO, misonyo na maneno maneno ni vitu vilivyozoeleka katika ndoa za mastaa duniani kote lakini kwa wale wa Kibongo, mateso ni maradufu kwani ukisikia ya moyoni mwao hasa kwa wale ambao hawajajaliwa kupata watoto, huwezi kuoa au kuolewa na staa.
Kupitia The Biggest IQ Paper, Ijumaa Wikienda, hii ndiyo ripoti kamili.

DOTNATA NA POSHI
Akiwa mjasiriamali na msanii maarufu Bongo, mwaka 2008, Husna Shaban ‘Dotnata’ alifunga ndoa na mwanajeshi mstaafu, Mohammed Ally ‘Poshi’na kupewa jina la Husna Poshi. Kufuatia maneno juu ya ndoa yake kutopata uzao, Dotnata alifunguka:

“Kusema kweli maneno yanaumiza lakini ni vema watu wakaelewa kuwa watoto na mali ni vitu vya duniani. Kitu ninachokiheshimu na kukifahamu ni kuwa kuolewa ni lazima lakini kuzaa ni majaliwa, unaweza kuolewa na usipate mtoto, hayo ni mapenzi ya Mungu, nawashauri watu wafanye kazi, waache maneno kwani hayajengi ghorofa.”

JIDE NA GARDNER
Akiwa msanii mkali wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo ‘Jide’ mwaka 2004 alifunga ndoa na aliyekuwa mtangazaji mkubwa wa Clouds FM, Gardner G Habash na katika safari hiyo kumekuwa na maneno lukuki juu ya suala la mtoto, huku mwanadada huyo akijitetea mara kwa mara:

“Kwa ambao wamekuwa wakinisema sana, kila siku mtoto... mtoto, wajue inaumiza sana na ukweli ni kwamba suala la mtoto, mbali na mipango ya wanandoa, pia ni jambo linalopangwa na Mungu.”

WASTARA NA SAJUKI
Wakiwa waigizaji wakali Bongo, mwaka 2009, Wastara Juma na Juma Kilowoko ‘Sajuki’, walifunga pingu za maisha na hadi leo wamepitia masengenyo mengi ambapo Sajuki alikuwa na haya ya kusema:

“Ukweli hakuna kitu kinachoumiza kama maneno maneno katika maisha ya binadamu, ni vema watu wakajua kuwa kila jambo lina mpango wake, wakati mwingine mtu unajitahidi kuwapuuza lakini si unajua moyo siyo chuma? Lazima upate maumivu.”

THEA NA MIKE
Kama ilivyokuwa kwa Wastara na Sajuki, Salome Ndumbagwe Misayo ‘Thea’, mwaka jana alifunga pingu za maisha na muigizaji mwenzake Michael Sangu ‘Mike’ na tayari wameshaumizwa na masengenyo, Mike alisema:

“Ni lazima ujifunze kuwapuuza watu wanaokusema vibaya hasa katika suala la kupata mtoto kwani kila kitu ni mipango ya Mungu. Ni kweli linaumiza sana. Mimi sijamuoa Thea ili nimzalishe watoto 10, kila kitu kina mpango wake.”

BESTA NA MARLAW
Hawa ni ‘maua’ kutoka katika fani ya Bongo Fleva, Besta Prosper na Lawrence Marima ‘Marlaw’ ambao walifunga ndoa hivi karibuni. Tayari wamekwishaanza kuulizwa vipi kuhusu mtoto. Marlaw alisema:

“Kwa kipindi kifupi tu, tayari tumeshaulizwa sana juu ya mtoto lakini ukweli ni kwamba wanatarajia kupata mtoto ‘soon’, hivyo mashabiki wetu wasijali.”

Na Gladness Mallya, GPL

No comments:

Post a Comment