Wednesday, July 27, 2011

Mahari ya WEMA hii hapa


MAHARI ya kumuoa Staa wa Filamu Bongo, Wema Issack Sepetu ni kubwa sana, hivyo kuwa tishio kwa mwanaume yeyote atakayethubutu kufunua kinywa chake na kutangaza ndoa na diva huyo anayesumbua vilivyo katika ulingo wa sinema nchini, Risasi Mchanganyiko lina mkoba wenye ‘documents’ zote kuhusu stori hii.

Akiongea kwa kujiamini katika ‘special interview’ juzi, pande za Sinza jijini Dar es Salaam, Wema alisema mwanaume ambaye anataka kumuoa lazima ajipange, kwa vile mahari yake si nyepesi.

KWA NINI MAHARI KUBWA?
Wema alisema, ukubwa wa mahari yake unatokana na vigezo bora alivyonavyo ambapo alivitaja baadhi kuwa ni uzuri wa sura, umbo na rangi kuwa ghali, hivyo hawezi kukubali kuolewa kwa pesa uchwara.

“Kama unavyoniona figa yangu namba nane, ni mzuri na ninavutia, sasa siwezi kukubali kuolewa kwa mahari ndogo, nataka mahari yangu ilingane na thamani niliyonayo,” alisema Wema bila kufafanua zaidi na kuongeza:
“Mimi toto la Kinyamwezi bwana, umbo langu linajionyesha hivyo muoaji lazima ajiandae...maana mahari si mchezo kabisa ni lazima ajikamilishe vizuri.”

Sifa nyingine aliyoitaja Wema kuwa inaongeza dau la mahari yake ni tabia njema aliyonayo, uvumilivu na upendo wa kweli kutoka moyoni hivyo mume wake atakuwa na uhakika wa kuishi maisha mazuri katika ndoa yake.

“Mimi ni mama bora, mwanaume atakayebahatika kunioa atakuwa amepata mke sahihi, si kwa uzuri wangu tu, bali mwenye uwezo wa kuhimili familia sawa sawa,” alisema.

MILA ZA KINYAMWEZI
Uchunguzi wa gazeti uliowashirikisha wazee wa kabila la Kinyamwezi, unaonesha kuwa uzuri wa sura, mvuto na rangi ni vigezo muhimu vinavyoongeza thamani ya mahari ya mwanamke.

Akiongea na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mzee mmoja wa Kinyamwezi aliweka wazi kuwa, mwanamke mwenye mvuto na mrembo huolewa kwa dau si chini ya ng’ombe 45 na kuendelea.

“Kwa mila za kwetu, zamani kama mwanamke ni mzuri sana, mwenye umbo zuri, halafu akawa mweupe lazima ulipe mahari ya ng’ombe 45 au zaidi ya hapo.

“Wanawake wa aina hiyo walipewa kipaumbele sana, wanaonekana wana thamani kubwa zaidi, kwa sababu wengi walikuwa wuesi,” alisema.
Hakuna ubishi kwamba mwonekano wa Wema ni mzuri, ana mvuto na ana kila sababu ya kuitwa mrembo kwa jinsi alivyo.

Ukiachana na umbo lake linalofanana na tarakimu ya namba nane kama alivyosema mwenyewe, Wema ana mwanya ambao unaongeza uzuri wake, rangi yake ya ‘chocolate’ pia nakshi nyingine ya uzuri wake usiofichika.

KUMUOA WEMA TSH. 15,750,000
Kauli ya Wema ukichanganya na maneno ya mzee wa Kabila la Kinyamwezi aliyezungumza na Risasi Mchanganyiko, mahari ya Wema inatakiwa kuanzia ng’ombe 35-45.

Ikiwa Wema atahitaji idadi ya ng’ombe 45 kama mahari yake, muoaji atalazimika kulipa kitita cha shilingi 15,750,000 (kumi na tano milioni, laki saba na hamsini elfu) ambayo ni hesabu ya ng’ombe hao kwa bei ya shilingi 350,000 (laki tatu na nusu) kila mmoja kwa bei ya sasa jijini Dar es Salaam.

Hata kama Wema ataamua kupunguza mahari yake hadi kufikia ng’ombe 20, bado muaoji atatakiwa kulipa kiasi cha shilingi 7,000,000 (milioni saba) fedha ambazo ni nyingi sana kwa mahari ukilinganisha na ugumu wa maisha uliopo.

Wema ni Miss Tanzania mwaka 2006, baada ya kuvua taji hilo aliingia katika tasnia ya filamu ambapo anafanya vyema hadi sasa.

Aidha, mrembo huyo ambaye haishi vituko na skendo kila wakati magazetini, kwa sasa ni mpenzi wa kinda anayewika katika muziki wa kizazi kipya, Abdul Naseeb ‘Diamond’ hivyo anapaswa kujiandaa kwa mahari hiyo kama ni kweli anataka kumchukua jumla.


Na Global Publishers TZ

No comments:

Post a Comment