Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
WANYOSHEANA VIDOLE KUMTAFUTA MCHAWI
KAULI tofauti zinazotolewa na viongozi wa Serikali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete na baadhi ya mawaziri kuhusu suala la mgawo wa umeme, zinaonyesha kutokuwapo uwajibikaji wa pamoja katika Baraza la Mawaziri.Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili kuhusu sakata la tatizo sugu la mgawo wa umeme nchini unebaini kwamba, kauli za viongozi hao wa Serikali hawana sauti ya pamoja hivyo kuongeza utata katika kulipati ufumbuzi wa kudumu suala hilo nyeti
Wengi wa wa walizungumzia sula hilo wamekuwa wakimnyoshea kidole Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuwa kiini cha tatizo.Hata hivyo, gazeti hili limebaini kuwa, mgongano huo unatokana na makundi mawili yanayotarajia kushiriki mbio za urais 2015, ambayo kila moja limekuwa likijaribu kutafuta umaarufu kisiasa na kujijengea himaya kwa umma.
Suala la Umeme
Akiwa katika maonyesha ya SabaSaba, Rais Kikwete alimkingia kifua waziri wake wa Nishati na Madini William Ngeleja kuhusu mgawo wa umeme akisema, tatizo hilo limetokana na mvua na Serikai haina namna ya kufanya.
Rais alifafanua kwamba, hakuna miujiza ambayo Serikali inaweza kufanya ili kumaliza tatizo hilo, kwani mabwawa yanayotegemewa kuzalizsha umeme, yamekauka.Kwa mujibu wa Rais Kikwete, haikuwa sahihi kumtuhumu Ngeleja kwa tatizo la ukame ambalo ni la Mungu na si la Serikali yake.Rais Kikwete alirudia kauli hiyo alipokuwa nchini Afrika Kusini wakati akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusu tatizo la umeme nchini.
Kauli ya Pinda
Hata hivyo, Kauli hiyo ya rais imeonekana kupishana na ile iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe, aliyehoji kwa nini Serikali isikubali ushauri wa kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia
tatizo la umeme.
Tofauti na Maelezo ya Rais Pinda alisema haoni umuhimu wa kufikia hatua hiyo, kwa vile Serikali haijashindwa kutatua tatizo la umeme."Tatizo letu ni hii mipango ya dharura, lakini kuhusu mipango ya muda mrefu ya kumaliza tatizo la umeme, Serikali haijashindwa. Naomba Mheshimiwa Mbowe ipe Serikali muda inaweza kulitatua tatizo hilo," alisema.
Kauli ya Sitta
Naye Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, akiwa mkoani Mbeya, aliweka bayana kwamba tatizo la umeme linatokana na uzembe serikalini.
Sitta alisema tatizo la mgawo wa umeme nchini limetokana pamoja na mambo mengine, ikwiamo Serikali kutojipanga vizuri kuwekeza katika nishati ya umeme.Sitta alisema yapo maeneo mengi ya msingi ya kimkakati ikiwemo maporomoko ya maji ya Stigler's, ambayo hayajapewa kipaumbele.Waziri Sitta aliweka bayana kwamba, miaka ya nyuma wakati wa Serikali ya Mwalimu Nyerere, mradi huo wa Stigler's haukuwa umepewa uzito kwa sababu ya mahitaji madogo, lakini sasa mahitaji ni makubwa.
Alienda mbali akisema tatizo la umeme siyo ukame kama inavyoelezwa bali ni mikataba ya kifisadi na uzembe, hivyo kusisitiza kuwa wote waliofikisha nchi ilipo kupitia mikataba
hiyo washitakiwe.
Waziri Ngeleja
Waziri Ngeleja alipopewa shinikizo la kujiuzulu baada ya bajeti yake kukataliwa alisema kwamba, hawezi kufanya hivyo kwa kuwa umeme sio tatizo lake pekee bali, Serikali nzima ya awamu ya nne.Ngeleja alisisitiza kuwa, kama ni suala la kuwajibika basi Serikali nzima inapaswa kufanya hivyo na sio yeye peke yake.Ngeleja alijitetea kwamba, tatizo kubwa linalosumbua katika suala la umeme ni bajeti finyu ya Serikali.
Waziri wa Fedha
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alipinga kauli ya Ngeleja akisema a ipo miradi mingi ambayo Waziri huyo wa Nishati na Madini angeweza kuibua kupitia wizara yake kwa ajili ya kumaliza tatizo la umeme.
Mkulo alisema wapo wawekezaji wengi wakiwemo kutoka China ambao wako tayari kuwekeza nchini bila kuhitaji hata shilingi moja ya Serikali ambao Ngeleja angeweza kuwatumia, lakini hakufanya hivyo.
Alitoa mfano kuwa walipotembelea China hivi karibuni, walikutana na baadhi ya wawekeza ambao walisema wako tayari kuja nchini kuwekeza katika sekta ya umeme bila kudia chochote kutoka Serikali ya Tanzania na kwamba Ngeleja analijua hilo.
Kashfa ya Rada
Mbali ya umeme, pia mawaziri wa Rais Kikwete wameonyesha kupingana kauli katika mambo muhimu kwa taifa, likiwamo sakata la ununuzi rada
Kwa muda mrefu viongozi Serikali wamekuwa wakieleza kuwa hakuna mtu anayehusishwa na kashfa hiyo nchini, lakini wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliweka bayana kuwa watuhumiwa wa sakata hilo nchini wapo.
Membe alisema mwishoni wakati akifanya majumuisho ya hoja ya bajeti ya wizara yake kwamba, hana mamlaka ya kuwataja watuhumiwa wa rada, lakini wapo.Kwa mujibu wa Membe, mamlaka ya kutaja watuhumiwa yako chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora (Mathias Chikawe).
Majibu ya Chikawe
Wakati Membe akimtupia zigo hilo, Chikawe, alijibu akisema hakuna mashitaka yeyote dhidi ya mbunge huyo wa Bariadi Magharibi.Kwa mujibu wa Chikawe, hakuna ushahidi wowote unaonyesha kwamba Chenge ana kesi ya kujibu.
Sakata la Dowans
Kuhusu sakata la rada, Sitta na Naibu Waziri, Dk Harrison Mwakyembe, pia walishawahi kuingia kwenye malumbano na Waziri Chikawe kuhusu malipo ya Sh 94 za tuzo ya kampuni ya Dowans, kabla ya suala hilo kupelekwa mahakamani.
Katika sakata hilo, Chikawe ambaye pia alionekana kuikingia kifua Dowans, aliwataka mawaziri hao ( Sitta na Mwakyembe) kuacha kuzungumza mambo nje ya vikao vya Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo, Sitta alijibu kwamba, hakuna mtu ambaye angeweza kumfunga mdomo katika sakata hilo, kwani msimamo wake ilikuwa ni kupinga malipo hayo ya Dowans.
CHANZO: MWANANCHI JULAI 27, 2011
No comments:
Post a Comment