Uongozi wa klabu ya Yanga umemwongezea majukumu kocha wao mpya, Hans Van Der Plyum raia wa Uholanzi kwa kumpa cheo cha Mkurugenzi wa Ufundi huku ukimtaka awasilishe kwa maandishi ripoti yake kila wiki.
Plyum ambaye amesaini mkataba wa miezi sita kuinoa Yanga ambao utamalizika Juni 30, tayari amejiunga na kikosi hicho kilichopo kambini nchini Uturuki, ambapo kilikuwa chini ya kocha msaidizi, Charles Boniface Mkwasa.
Akizungumza jijini jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga alisema wameamua kumpa Ukurugenzi wa Ufundi kocha huyo wakiamini kuwa anaweza kufanya kazi yake kama kocha na kutekeleza majukumu hayo mengine ndani ya klabu.
“Tunamwamini kocha wetu mpya, anaweza kutekeleza majukumu yake, lakini tunachokitaka ni uongozi kuwa karibu na benchi la ufundi na tulichokiamua ni kocha kutuletea ripoti ya mwenendo wa timu tena kwa maandishi na siyo kwa maneno kama ilivyokuwa awali kila wiki,” alisema Sanga.
Alisema kocha huyo amewasili nchini Uturuki na lengo la kumpeleka huko saa chache baada ya kusaini mkataba ni kuungana na timu hiyo na kuendelea na programu aliyoanza nayo kocha msaidizi Mkwassa ambaye anatarajiwa kurejea nchini keshokutwa Jumamosi.
“Mkwasa ana matatizo ya kifamilia na Januari 18 atarejea nchini, hivyo tumeona ni vyema kocha Plyum akawa naye kwa siku hizo chache na kumpa programu alizoanza nazo ili yeye aendelee hapo baada ya Mkwasa kuondoka kambini,” alisema Sanga.
Akizungumzia hatima ya kiungo wa timu hiyo, Athuman Iddi ‘Chuji’, Sanga alisema suala lake limepelekwa kwenye kamati yao ya nidhamu ya Yanga ambayo itakaa na uongozi kuona nini cha kufanya juu ya mchezaji huyo aliyesimamishwa kwa muda usiojulikana kwa kile kilichodaiwa ni utovu wa nidhamu.
“Uongozi haupo kwa ajili ya kutoa adhabu ya kumkomoa mchezaji, Chuji ameleta barua ya kuomba msamaha hivyo uongozi bado unalijadili suala lake ambalo lipo chini ya kamati ya nidhamu,” alisema Sanga na kuongeza kitendo cha Chuji kuachwa safari ya Uturuki ni adhabu tosha.
Wakati huo huo, Yanga imewataka wanachama ambao hawajalipia ada zao kufanya hivyo ili wapate haki ya kushiriki kwenye mkutano mkuu utakaofanyikaJanuari 19.
- Mwananchi
No comments:
Post a Comment