Friday, January 17, 2014

East Coast Team kufufuliwa upya


KUNDI la muziki wa Bongo Fleva la East Coast Team (ECT) lililowahi kuwika vilivyo nchini likiundwa na wasanii mahiri kabla ya kusambaratika kutokana na sababu kadha wa kadha, kwa sasa lipo mbioni kurejea upya kuendeleza makamuzi.

Kundi hilo lililokuwa likiundwa na wasanii wanaotamba hadi leo kama Ambwene Yesaya ‘AY’ Hamis Mwinjuma ‘mwana FA na Gwamaka Kaihula, ‘King crazy GK,’ lipo kwenye maandalizi ya kuibuka upya kivingine kwa lengo la kurejesha heshima yake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, GK aliwataka mashabiki wa kundi hilo kukaa mkao wa kula baada ya wasanii wenzake kumpa shavu katika kazi zake anazoziandaa ikiwemo kujipanga kwa kundi hilo kurejea.

GK alisema kuwa kwa sasa wameanza kuongeza nguvu kwa kulirudisha kundi hilo ambapo alieleza kuwa wanahitaji wanaume wawili na msichana mmoja, na kujigamba kuwa tayari ECT wameshaingia studio kupika ngoma mpya ambayo anaamini itafanya vizuri.

“Baada ya wote kupata elimu sasa tutatumia elimu tuliyoipata kuhakikisha ladha ya muziki inadumu na inapedwa zaidi na mashabiki, kwa hiyo tunachotaka sasa ni kuiweka ECT kwenye level nyingine na si ya zamani, watu wamuone GK anavyopiga kinanda na gitaa,” alisema.

Hilo ni kundi lililowahi kutesa na nyimbo mbalimbali ikiwemo ya ‘Nitakufaje, Sister sister na Hii leo.

- Happiness Mnale, Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment