Wednesday, May 30, 2012

Watatu Simba mbioni kwenda Yanga


KATIKA hali ya kujiimarisha kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu, klabu ya Yanga imepanga kuivamia kambi ya Simba na kusajili wachezaji watatu wa kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wapya wa Bara.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani za Kamati ya Usajili ya klabu hiyo zilizopatikana jana, zimewataja wachezaji hao kuwa ni beki wa kati, Juma Nyoso, Juma Jabu na kiungo chipukizi Uhuru Selemani.

Habari zaidi zinadai kuwa, Wanajangwani wako tayari kumwaga kiasi kikubwa cha pesa ili kuwanasa nyota hayo walioiwezesha Simba kutwaa ubingwa msimu huu kabla ya ligi kumalizika.

Mtoa habari amepasha kuwa, tayari mazungumzo ya awali yamefanyika na kinachosubiriwa ni uamuzi wa wachezaji hao kukubali ofa na kisha kusaini mikataba.

“Tumeshafanya mazungumzo ya awali, kwa sasa hatuwezi kuweka wazi kila kitu lakini tunachosubiri ni wao kukubali kusaini mikataba kwa ajili ya msimu ujao," alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa vile siyo msemaji.

"Tunaamini kama tutawapata, basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika usajili kwa ajili ya msimu ujao," alisema zaidi.

Aidha, alisema mbali na wachezaji hao pia wana mpango wa kusajili wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Rwanda waliong'ara wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka jana.

Wachezaji hao ambao ni 'mapacha' wa ushambuliaji wa klabu ya APR ni Meddie Kegere na Olivier Karekezi.
"Kwa sasa hatuna tena tatizo na pesa za usajili, tuna kila uwezo wa kumsajili mchezaji tutakayemtaka," alisema mtoa habari.

Juhudi za kuwatafuta wachezaji hao kuthibitisha madai ya Yanga zilindikana isipokuwa mchezaji Uhuru aliyesema: "Nachoangalia ni maslahi niko tayari kwenda timu yoyote itakayonihitaji na kufika dau."

Aidha, alisema anashangaa uongozi wa Simba kuwa kimya bila kusema lolote mpaka sasa wakati wanafahamu mkataba wake umefika tamati.

"Sina mkataba na Simba kwa sasa na sijaona jitihada zozote za viongozi wala sijapigiwa simu kufahamishwa kama nitaendelea kubaki ama naondoka. Niko huru naangalia atakayekuja na dau kubwa," alisema.

Uhuru ameichezea Simba karibu misimu mitatu.

Jessca Nangawe na Sweetbert Lukonge

No comments:

Post a Comment