Wednesday, May 30, 2012

Redds Miss Tanzania mwisho Juni 4


KAMATI ya Redd's Miss Tanzania imesema Juni 4, itakuwa mwisho wa kurudisha fomu kwa warembo wanaotaka kushindana katika shindano dogo la kumsaka mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Dunia (Miss World 2012).

Mkurugenzi wa Lino International Agency waandaaji wa mashindano hayo, Hashim 'Uncle' Lundenga alisema wanatarajia kufanya mchujo wa washiriki Juni 5.

Lundenga alisema katika mchujo huo watabaki warembo 10 ambao wataingia fainali ili kupata mmoja atakayeiwakilisha nchi kwenye mashindano Dunia yatakayofanyika Agosti 18 kwenye ukumbi wa Dongsheng Fitness Center Stadium, mjini Ordos, Inner Mongolia, China.

Lundenga alisema kuwa zoezi hilo lilisimamishwa hapo awali kutokana na kuzuiwa na serikali kipindi ambacho tayari warembo 12 walikuwa wamekwisha chukua fomu za kushiriki.

"Mchakato umeanza na tayari tumepewa baraka kutoka Serikalini," alisema Lundenga na kuongeza kwamba watataja tarehe mpya ya mashindano hivi karibuni.

"Fomu za kuomba kushiriki zinapatikana katika ofisi za Miss Tanzania jijini Dar es Salaam na mawakala wote wa mashindano hayo katika mikoa ya Tanzania Bara hivyo ni nafasi kwa warembo kujitokeza kuchukua fomu za kinyang’anyiro hicho na kuzirudisha kabla ya Juni 4.," alisema.

Alisema amefurahishwa na kasi ya kuchukua na kurejesha fomu, hata hivyo wanahitaji warembo wengi zaidi ili kuweza kupata wigo mpana kwa ajili ya kumsaka mrembo atakayewania taji la Dunia ambalo kwa sasa lipo mikononi mwa mrembo kutoka Venezuela, Ivian Sarcos.

Hadi sasa jumla ya nchi 84 zimekwishapata wawakilishi wao kwa ajili ya mashindano hayo huku nchi 32 ikiwamo Tanzania zikiwa bado hazijapata wawakilishi, hali hiyo imekuja kulingana na mabadiliko ya kalenda ya mashindano ya urembo ya dunia.

Imani Makongoro, Mwananchi

No comments:

Post a Comment