Tuesday, December 27, 2011

Ripoti kamili ya Mafuriko DAR!

JANGA la mafuriko lililolikumba Jiji la Dar es Salaam baada ya mvua kubwa iliyoambatana na radi kunyesha Desemba 20 na 21, mwaka huu, ndiyo habari ambayo inaitikisa nchi, hii ni ripoti kamili ambayo huwezi kuipata popote zaidi ya Gazeti la Uwazi.
Baadhi ya wakazi wana hali mbaya, wengine wamepotelewa na ndugu zao hivyo kuifanya Krismasi yao kuwa mbaya kutokana na majonzi mazito waliyonayo.
Timu ya Uwazi iliingia mitaani kwa siku tano mfululizo tangu siku ya tukio na kukusanya mambo mengi ambayo yanatia simanzi.
Zipo familia ambazo kwa sasa hazina makazi, maisha yao ni magumu, kila kitu wameanza upya baada ya madhara hayo ya mafuriko.

HARUFU BONDE LA MSIMBAZI
Taarifa ya serikali iliyotolewa wiki iliyopita inaeleza kwamba, idadi ya watu waliofariki imefikia 38, huku wawili kati yao wakiwa hawajatambuliwa, lakini Uwazi limeelezwa kwamba waliokufa ni wengi zaidi.
Kwa mujibu wa wakazi wa maeneo ya Jangwani na Kigogo, wamesema kwamba kuna hofu ya kuwa wamekufa watu wengi zaidi ya idadi iliyotajwa na serikali hasa kutokana na harufu kali iliyopo katika Bonde la Msimbazi.
“Harufu ni kali, bila shaka kuna watu wengine ambao wamo chini, serikali inapaswa kutumia vifaa vya kisasa kwa ajili ya kukagua eneo hili ili kujua kama kuna maiti nyingine,” Ali Rashid, mkazi wa Kigogo, Dar aliwaambia waandishi wetu.
Joseph Lucas aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Jangwani, alisema: “Kwa hali ilivyokuwa ni vigumu kuamini kuwa wamekufa watu 38 pekee. Inaweza kuwaingia akilini watu ambao hawaishi maeneo haya, lakini sisi ndiyo tunajuana.
“Ipo haja ya serikali kufanya uchunguzi zaidi, harufu inayotoka Bonde la Msimbazi ni ishara tosha kwamba kuna maiti zipo chini. Halmashauri ya Jiji inapaswa kuingia kazini ili tuwe na uhakika na ndugu zetu.”

WAFARIKI FAMILIA NZIMA
Habari ya kusikitisha zaidi ni kwamba, ipo familia ya watu watano, wakazi wa Vingunguti Dampo wamefariki dunia kutokana na madhara ya mafuriko hayo.
Watu hao ni Severina Luhwagila (27), Bakari Kihoo (10), Agnes Kihoo (5), Jeremia Kihoo (5) na Nehemia Lubida ambaye umri wake haukutajwa.
Severina ndiye mama wa familia hiyo yenye watoto watatu, Bakari, Agnes na Jeremia ambapo Nehemia ni msaidizi wa kazi za nyumbani.
Akisimulia kisa hicho, jirani wa familia hiyo, Jackson Geka, alisema: “Ilikuwa ni alfajiri ya Desemba 20, mwaka huu, nilisikia mvua kubwa ikianza kunyesha. Sikuweza kulala tena, nikatulia nikisikilizia, maana ni wazi niliona hatari kubwa mbele yangu.
“Ghafla nikaona maji yakiingia ndani, kwa tahadhari nikaanza kuitoa familia yangu na kuihamishia sehemu nyingine. Niliporudi asubuhi nikaanza kuangalia mazingira. Nilishtuka sana kuona nyumba yangu na ya jirani yangu zimeanguka kabisa.
“Nilianza kuhaha kuwatafuta, lakini sikufanikiwa kwa vile sikuwa na vifaa vya kuzamia kwenye maji. Baadaye nikaambiwa na majirani zangu kwamba walisombwa na mafuriko.”
Geka alisema, maiti nne zilipatikana baadaye, isipokuwa moja ya Bakari ambaye jitihada za kuutafuta mwili wake bado zinaendelea.

BABA WA FAMILIA
Akizungumza na Uwazi akionekana dhahiri kuwa na majonzi mazito, baba wa familia hiyo iliyopotea yote aitwaye Erasto Kihoo (27), alisema ana maumivu makali moyoni mwake, kwani amepoteza nyumba na familia yake kwa jumla.
“Nimeteseka sana na maisha, hatimaye mimi na marehemu mke wangu tukadunduliza na kupata kakibanda ketu (nyumba), lakini leo hii nimepoteza kila kitu. Mke wangu, wanangu na msichana wangu wa kazi. Nina majonzi mazito sana.
“Si rahisi kuelezea kwa mdomo jinsi ninavyoteseka na kuungua moyoni, lakini Mungu aliye juu ndiye anayeona mateso yangu,” alisema Kihoo akijizuia kutoa machozi, lakini alishindwa.
Kihoo hakuwepo siku ya tukio, ambapo alisema alikuwa safarini Iringa alipokwenda kumtembelea baba yake mzazi aliyekuwa mgonjwa sana.
“Naumia sana, maana inawezekana kama ningekuwepo, ningeokoa familia yangu. Sijui nitaanzia wapi?” alisema akizidi kulia.
Alisema, alisafiri siku moja kabla ya tukio (Desemba 19, mwaka huu) ndipo nyuma yakatokea maafa hayo ambayo yamemuachia maumivu makali sana maishani mwake.
Anaendelea kusimulia kwa uchungu: “Mpaka siamini kilichotokea, namaliza mwaka nikiwa sina mke tena wala watoto. Mungu anipe ujasiri, kwa nguvu zangu siwezi. Sitaweza...siwezi kabisa.”

MAAFA MENGINE
Wakati huohuo, mkazi mwingine wa Vingunguti, Hamis Kasimu Nyau,19, ameripotiwa kufariki katika mafuriko hayo.
Akisimulia chanzo cha kifo cha Hamis, mama mzazi wa marehemu huyo aitwaye Jamila Malunda, alisema mwanaye alifariki alipokuwa akifanya jaribio la kuvuka Mto Msimbazi uliojaa maji kwa ahadi ya kupewa Tsh. 1500.
“Kuna kijana alimwambia avuke mto kama anaweza, kwa malipo ya 1500, sasa kwa sababu alizihitaji hizo fedha bila kujua madhara ambayo angeweza kuyapata, akakubali kuvuka, lakini kwa bahati mbaya hakutoka,” alisema mama Malunda.
Aliongeza: “Siamini kama 1500 tu ndiyo imemtoa uhai mwanangu. Yaani nina majonzi sana.”
Kijana mwingine aliyepoteza maisha ni Nia Abdallah,19, mkazi wa Buguruni Kwa Mnyamani ambaye alikuwa katika harakati za kujikoa lakini alisombwa na maji na kuokotwa katika mto unaounganisha Mto Msimbazi.

Mafuriko hayo pia yamesababisha majonzi kwa familia nyingine ya Buguruni Kisiwani baada ya kijana wao mpendwa Ariro Masiku, 28, kufariki baada ya kuzolewa na maji.
Habari zinasema kuwa Ariro ambaye alikuwa anafanya kazi ya ulinzi katika kampuni moja jijini Dar es Salaam, alifariki dunia Desemba 21, mwaka huu, saa 5:40 asubuhi wakati akitoka kazini.
Marehemu Ariro aliteleza kwenye maji yaliyokuwa yakienda kwa kasi wakati akiangalia wakazi wa Buguruni walioathirika na mvua hizo wakihama kwenye maeneo yao kukimbia hatari.
Marehemu Ariro ameacha mke, Jessica Ariro na watoto wawili, Latifa na Debora, ambao kwa sasa wapo kwa mjomba wao Mbagala, Dar.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa wakati wowote kutokea juzi Jumapili, kwenda kijijini kwao Lolwe, Nyaongo, Wilaya ya Rorya mkoani Mara kwa mazishi.

FAMILIA HII NAYO HAKUPONA MTU
Kigogo, Dar es Salaam, waandishi wetu walioneshwa nyumba nyingine ambayo ilidaiwa kuwa hakupona hata mtu mmoja.
Jirani wa nyumba hiyo, Samuel aliliambia Uwazi kuwa familia ya Mzee John, hakuna aliyenusurika kwenye mafuriko hayo.
“Sisi majirani tunaamini wote wamekufa kwa sababu hata nyumba imezolewa na watu wote waliokuwa wanaishi kwenye nyumba hiyo hawajaonekana mpaka leo,” alisema Samuel na kuongeza:
“Ile nyumba ilikuwa na watu kama saba hivi akiwemo mwenye nyumba, tunafuatilia lakini hakuna matumaini kama wapo salama.”

MAONI YA WANANCHI
Wakizungumza na Uwazi kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, wananchi wa Vingunguti walisema wameshangazwa na serikali kwa kutokuwa nao bega kwa bega katika maafa hayo.
“Nilitegemea serikali ingetoa misaada ya magari ya kubebea miili ya marehemu kwenda kuzika, maji ya kunywa, vyakula au hata baadhi ya viongozi kuhudhuria maziko, lakini jambo hilo halikufanyika.
“Sisi watu wa Vingunguti tunaona kwamba serikali imetusahau kabisa kama vile sisi siyo Watanzania. Tumeumizwa sana na hilo, lifikishe hili ndugu mwandishi, tunajua watasoma,” alisema mkazi mmoja wa Vingunguti Dampo.


Na Haruni Sanchawa na Makongoro Oging, GPL

No comments:

Post a Comment