Friday, November 18, 2011

KONA YA MKUBWA KAMBI: Dawa ya Mama Mkwe!


Hapo zamani za kale huko China, Binti aitwaye Li-Li aliolewa, yeye na mume wake wakaenda kuishi kwa mama wa mume wake yaani mama mkwe.

Kwa muda mfupi tu walioishi Li-Li aligundua kwamba yeye na mama mkwe hawaendani kabisa, walitofautiana kwa kila kitu na Li-Li alikasirishwa sana na tabia za mama mkwe wake kwani mama mkwe alikuwa anamlaumu (criticize) muda wote.

Siku zilipitia, wiki zikapita na miezi ikapita kila siku Li-Li na mama mkwe ni kuzozana na kushambuliana, kibaya zaidi ni kwamba kutokana na traditions za Uchina ilimpasa Li-Li kumpigia goti kila lile ambalo mama mkwe alihitaji afanye na ukweli hali mbaya ya mahusiano kati ya Li-Li na mama mkwe ilimfanya hata mume wake Li-Li kujisikia vibaya sana.

Mwisho Li-Li hakuweza tena kuvumilia tabia mbaya na utawala wa imla wa mama mkwe hivyo akaamue kufanya kitu, hivyo akafunga safari kwa rafiki wa baba yake ambaye alikuwa anaitwa Mzee Huang ambaye alikuwa anauza dawa za kienyeji (herbs).

Alipofika kwa mzee Huang akamweleza yote anayokutana nayo na kwamba anaomba msaada kama anaweza kumpa sumu ili aweze kumuua yule mama mkwe na kuondokana na lile tatizo milele (once and for all)

Mzee Huang akafikiria kwa muda na mwisho akamwambia Li-Li atamsaidia kulimaliza tatizo lake ingawa Li-Li alitakiwa kusikiliza kwa makini na kutii kile ataambiwa akafanye.

Na Li-Li naye kwa furaha akajibu kwamba nitafanya chochote utaniambia nifanye.
Ndipo Mzee Huang akaingia ndani na kutoka na mfuko uliosheheni dawa (herbs) na akaanza kumpa maelezo Li-Li:
"Huwezi kutumia sumu ya haraka kumuua mama mkwe wako kwani kila mmoja atakutilia mashaka (suspicious) wewe hivyo nimekupa kiasi cha kutosha cha dawa (herbs) ambayo itatumika kidogo kidogo na kujenga sumu ya kutosha na hatimaye kumaliza.

Hivyo kila siku tengeneza mlo safi na weka dawa kidogo kwenye hicho chakula.
Sasa, ili kila mtu asikutilie mashaka wewe hasa akifa lazima uwe makini sana kujifanya rafiki kwake, usibishane naye na kubali chochote anakwambia na umuhudumie kama vile ni malkia, si unajua ipo siku atapotea kabisa”.

Li-Li alikuwa na furaha ya ajabu, akamshukuru mzee Huang na akaenda nyumbani kuanza shughuli ya kumuua mama mkwe wake.

Miezi ikapita, wiki zikapita na siku zikapita, Li-Li aliendelea kumpa mama mkwe chakula chenye ile sumu na alikuwa anakumbuka sana jinsi Mzee Huang alivyokuwa amemweleza jinsi ya kuepuka kutiliwa mashaka, hivyo aliweza kujizua hasira zake na alimtii mama mkwe kwa kila kitu na alimhudumia kama mama yake mzazi (malkia)

Baada ya miezi sita, nyumba nzima ilibadilika baada ya Li-Li kuweza kizishinda hasira zake kwa mama mkwe na kumtii na wakajikuta hawagombani tena na hawakuweza kuzozana au kubishana kwa miezi sita mfululizo na wakajikuta wanaelewana na kuishi vizuri.

Pia mtazamo wa mama mkwe nao ulibadilika na alianza kumpenda Li-Li kama binti yake mwenyewe na akawa anawasilimua rafiki zake mwenyewe kwamba Li-Li alikuwa ni binti mzuri mwenye tabia njema ambaye hakuna mama mkwe duniani anaweza kumpata. Li-Li na mama mkwe wakawa ni kama mama na binti yake.

Pia mume wa Li-Li alikuwa na furaha ya ajabu alipoona kile kinatokea katika familia.
Ndipo Li-Li akarudi kwa mzee Huang kuomba masaada tena, akamwambia mzee Huang;
“Tafadhari nisaidie jinsi ya kuiondoa ile sumu isimuue mama mkwe kwani amebadilika na amekuwa mwanamke mwema sana kwangu na ninampenda kama mama yangu mzazi na sitapenda afe kwa sababu ya sumu niliyompa”.

Mzee Huang akawa anatabasamu huku anatikisa kichwa.
“Li-Li huna haja kuwa na mashaka au kuogopa, sikukupa sumu yoyote, dawa niliyokupa ilikuwa ni vitamins kwa ajili ya kuimarisha afya. Sumu kubwa iliyokuwepo ilikuwa kichwani mwako (mind) na mtazamo wako kuhusu mama mkwe na hiyo sumu yote imesafishwa na upendo ambayo umeutoa kwake”.

Je, rafiki zangu mmegundua kwamba jinsi unavyowahudumia wengine ndivyo na wao watakavyokuhudumia wewe.

Kuna msemo wa kichina ambao unasema:
"The person who loves others will also be loved in return."

Inawezekana ni kweli unasuguana sana na mama mkwe au mume wako au mke wako au mpenzi wako na tatizo kubwa ni mtazamo wako kuhusu yeye na ungeamua kumpenda na kumhudumia kama malkia au mfalme mambo yangebadilika.


Na Mkubwa Kambi (Maisha na Ushauri)

No comments:

Post a Comment