Na Saleh Ally
USHINDANI wa Yanga na Simba unarejea tena kwenye mvutano mkubwa huku dalili zikianza kuonyesha mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya watani hao Oktoba 29, itakuwa ni vita kuu.
Hali hiyo inatokana na kila upande kuwarejesha wapiganaji wake hivyo kufanya mambo yawe magumu au rahisi kwa kila upande.
Yanga wako katika hatua za mwisho kumalizana na milionea Yusuf Manji ili aendelee kuifadhili klabu hiyo lakini Simba tayari wamewarudisha wapiganaji wa kundi la Friends Of Simba (FOS) kupitia kamati ndogo ndogo, ndani yake zikiwemo sura mpya katika soka, lakini ni machachari.
Iwapo Manji ataanza kuifadhili Yanga, hakika ushindani utakuwa mkubwa na kuifanya mechi hiyo ya Oktoba 29 kuwa vita kuu, Tayari ameshatangaza kutaka kuanza kwa kumuua Myama. Lakini inaonekana FOS hawatakubaliana na hilo hata kidogo.
Simba wameunda Kamati za Fedha, Mashindano, Ufundi, Usajili na Nidhamu. Baadhi ya kamati hizo zinawajumuisha wakali kama Kassim Dewji, Azim Dewji, Hassan Hassanoo, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Mohammed Nassor, Evans Aveva, Musley Ruwey, Jamal Rwambo, Crescentius Magori na Haspope.
Lakini kuna wabunge maarufu kama Zitto Kabwe (Chadema), Amos Makala, Murtaza Ally Mangungu, Richard Ndassa (wote CCM).
Ushindani:
Friends of Simba inayoongozwa na watu kama Kassim Dewji ‘Injinia’, Hassan Hassanoo ‘Mpiganaji’ wamekuwa na sifa ya kuiongoza Simba kuifunga Yanga mfululizo. Lakini baada ya Manji kuingia Yanga, upepo ulibadilika na Jangwani wakawa wababe na kufuta uteja wa miaka saba mfululizo.
Maana yake, Oktoba 29 kila upande utataka kuonyesha kwa mashabiki wake kuwa kwa nini umerudi.
Hofu:
Kila upande utakuwa na hofu, huenda mamilioni na mipango ya Manji ikawa ni hofu kuu Msimbazi. Lakini Jangwani wanajua FOS wasivyolala na kukesha kama ‘popo’ ili mradi wadondoshe ukutwa wa Jangwani.
Hofu inachanganywa na uwezo wa mipango lakini kila upande utahofia hongo kupenyezwa ili wahujumiwe.
Fedha v Vichwa, mipango
Ingawa upande wa Friends of Simba kuna watu wenye uwezo wa kifedha, wanajua hakuna atakayegusa ‘kisu’ cha Manji. Upande wa Manji pia kuna mipango lakini inajulikana FOS ni kiboko kwa mipango ya kuwaua Jangwani.
Lakini FOS wameongeza watu wenye mipango zaidi, mfano Zitto Kabwe na Amos Makalla ingawa wako kwenye kamati tu lakini lazima wanaweza kutoa mbinu au michango yao kuhakikisha Oktoba 29, furaha inapotea Jangwani.
Jana Mwenyekiti, Ismail Aden Rage alikutana na wajumbe wa kamati alizoziteua na wote wameahidi ni lazima wauiue Yanga siku hiyo ikiwa ni sehemu ya kuanza kazi yao.
Pamoja na kuwa na mechi kabla ya kukutana, mechi dhidi yao imeanza kuwachanga watani, Simba wameanza kambi Bamba Beach, Kigamboni na Yanga wanajiandaa kuondoka Jangwani na kuhamia kusikojulikana!
No comments:
Post a Comment