KLABU ya Seattle Sounders ya Marekani ambayo ilimfanyia majaribio ya kucheza soka la kulipwa kiungo wa Azam, Mrisho Ngassa kisha kuelezwa kuwa amefaulu, imeipa wakati mgumu Azam kutokana na kuwa kimya juu ya usajili wa mchezaji huyo.
Katibu Mkuu wa Azam, Idrisa Nassor ameliambia Championi Ijumaa kuwa hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea baina yao na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ikiwa ni miezi michache baada ya mchezaji huyo kurejea nyumbani kutoka katika majaribio hayo.
“Sisi tunausubiri ujio wao kwa maana kama ni suala la majaribio tumelimaliza kwa mafanikio, kwa maana hiyo kazi iliyobakia kwao ni kufanya mazungumzo ya mwisho na kumaliza jambo hili lakini hawaonyeshi dalili yoyote.
“Ngassa ni mchezaji wetu tunayemtegemea na mafanikio yake ndiyo mafanikio ya klabu, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya soka letu.
“Si unajua hata kama itakuwa nyumbani ukiwa na binti ametokea mchumba kutoa barua huwezi ukamuuliza atakuja lini kuoa na ndiyo ilivyo kwetu hatuwezi kuwauliza, tunavuta subira,” alisema Nassor.
Ngassa aliyesajiliwa kutoka Yanga kwa ada ya Sh milioni 90 alienda Marekani kufanya majaribio hayo na moja kati ya mechi yake kubwa akiwa huko ni kucheza dhidi ya Manchester United.
Na Khadija Mngwai, Global Publishers Tz
No comments:
Post a Comment