WABABE kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), TP Mazembe wametangaza kuwa klabu yoyote inayomtaka mshambuliaji wao kinda, Mbwana Samatta italazimika kutoa kitita si chini ya dola 700,000 (Sh bilioni 1.1).
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Mipango wa TP Mazembe, Frederic Kitenge alisema hawajamuweka sokoni mshambuliaji huyo lakini kama itatokea timu inataka kumnunua hawatakuwa tayari kumuuza chini ya fedha hiyo.
“Hatujamuingiza sokoni, unajua hajamaliza hata msimu lakini thamani yake haiwezi kuwa chini ya dola 700,000 kutokana na sababu nyingi sana,” alisema Kitenge.
“Tokea amekuja hapa Lubumbashi, Mbwana anaonekana atakuja kuwa mchezaji mkubwa sana. Kwa kuwa ni mapema naweza kusema si chini ya thamani hiyo.
“Lakini kadiri siku zinavyokwenda basi thamani yake itaongezeka, ninaamini ni kati ya wachezaji watakaouzwa kwa thamani kubwa na ana nafasi ya kupata mafanikio makubwa hapo baadaye.”
Miezi michache iliyopita, mabingwa hao wa zamani wa Afrika walitoa dola 150,000 (Sh milioni 240) kwa Simba ili kumnasa Samatta aliyekuwa amejiunga na timu hiyo siku chache akitokea African Lyon.
Hivi karibuni, klabu kadhaa za Ubelgiji na Ufaransa zilianza kumzungumzia Samatta ikiwa ni pamoja na kutuma wawakilishi wao kwa ajili ya kumshuhudia akikipiga katika ligi ya nchi hiyo.
Samatta amekuwa lulu, akionyesha uwezo wa juu huku akishirikiana kwa karibu na nyota wa timu hiyo, Tresor Mputu ambaye amerejea kutoka kifungoni.
Mputu alimpiga mwamuzi wakati wa michuano ya Kombe la Kagame katika mechi dhidi ya APR, mwaka jana nchini Rwanda. Shirikisho la Soka Afrika (Caf), likamfungia kucheza soka kwa mwaka mmoja.
Na Saleh Ally, Global Publishers Tz
No comments:
Post a Comment