Saturday, July 9, 2011

Hayawi, hayawi......Yametimia


BAADA ya miaka 19, mabingwa wa Tanzania, Yanga watakutana na mabingwa wa kihistoria wa Kagame Castle Cup, Simba kwenye fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa klabu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Ushindi wa Yanga wa penalti 5-4 dhidi ya St George ya Ethiopia unafanana na ule iliyopata Simba dhidi ya El Merreikh ya Sudan na kutimiza ndoto za watu wengi hususani Cecafa waliokuwa wakiomba usiku na mchana ili miamba hiyo ya Tanzania iweze kucheza fainali.

Jambo la kuvutia zaidi kwenye fainali hiyo ni kwamba itawakutanisha makocha wa Kiganda, Sam Timbe aliyechukua taji hilo mara tatu dhidi ya Moses Basena mwenye ndoto ya kunyakuwa taji hilo kwa mara ya kwanza akiwa na Simba.

Pia, Yanga na Simba mara ya mwisho walikutana kwenye fainali ya michuano ya Kagame mwaka 1992 ambapo vijana hao wa Jangwani walipoteza kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar. Mashabiki wa Yanga wakiwa na kumbukumbu ya penalti ya mwisho iliyopigwa na David Mwakalebela na kutoka nje.

Mabingwa hao Tanzania jana wakicheza mbele ya mashabiki wao wachache iliwabidi kusubiri hadi penalti ya mwisho iliyopigwa na Anthony Bongole na kugonga mwamba na kurudi uwanjani na mwamuzi Denis Batte kutoka Uganda kusema siyo goli.

Katika changamoto hiyo ya mikwaju ya penalti nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ndiye aliyekosa kabla ya Nadir Haroub kufunga kwa shuti lililogonga mwamba na kutua ndani ya mstari wengine waliopata ni Juma Seif, Davies Mwape, Hamisi Kiiza na Nurdin Bakari aliyepiga penalti ya mwisho kama ilivyokuwa kwa mechi dhidi ya Red Sea wakati wa mechi robo fainali.

Kwa upande wa St George waliopata ni Degu Debebe, Abebawa Butako, Isaac Isinde na Adane Girma waliokosa ni kinara wa ufungaji wa michuano hiyo Said Salahdin aliyepaisha na Bongole.

Beki Oscar Joshua alifanya kazi kubwa ya kumwangusha nje kidogo ya eneo la hatari mshabuliaji hatari wa St George, Said Salahdin aliyewatoka mabeki dakika 115 na kujikuta akipewa kadi ya njano.

Mchezo ulianza kwa kasi Yanga kujaribu kufanya mashambulizi ya nguvu na kujaribu kuwachanganya St George wanaosifika kwa kuwa na safu bora ya ushambuliaji.

Umakini wa ngome ya Yanga chini ya Nadir Haroub na kipa Yaw Berko uliwafanya mabingwa hao wa Tanzania kufanikiwa kupata suluhu hadi mapumziko.

Mwanzoni mwa mchezo huo kinara wa ufungaji wa michuano hiyo Said Salahdin alikosa bao la wazi baada ya Nadir na Chacha Malwa kujichanganya, lakini kipa Berko alifanikiwa kuokoa hatari hiyo.

Kocha wa Yanga, Sam Timbe alifanikiwa kuharibu mipango ya St George kwa kutumia mfumo wa 4-4-2 dhidi ya ule wa Mtaliano Giuseppe Dossena aliyetumia mfumo wa 4-3-3.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili shuti la Shadrack Nsajigwa aliyekuwa kwenye kiwango cha juu jana alipiga shuti na kupenya kwenye nyavu iliyochanika dakika 46, lakini mwamuzi alikuwa makini kuona hilo na kusimamisha mchezo kwa dakika 9, ndipo kamba ya katani ilipotumika kushona sehemu iliyochanika.

Godfrey Taita alikosa bao baada ya kichwa chake kupaa juu dakika ya 56, akiunganisha krosi ya Oscar Joshua.

Kocha Timbe aliwatoa Kiggi Makasi na Jerryson Tegete na kuwaingiza Hamisi Kiiza na Rashid Gumbo ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.

Kwa mara ya kwanza katika mechi zote za Yanga ilizocheza uwanjani hapo katika mashindano hayo mashabiki wake walikuwa wachache yote kutokana na hofu ya timu yao kufanya vibaya.

Yanga na Simba ziliumana Machi 5 mwaka huu na kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2010-2011 uliofanyika uwanja wa taifa, lakini katika msimu huo katika mchezo wa awali uliofanyika Oktoba 16 mwaka jana, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Pia timu hizo zilikutana mwaka huu Januari 11 katika mashindano ya kombe la Mapinduzi, ambapo Simba ilishinda mabao 2-0 na kutwaa kombe la Mapinduzi kwenye uwanja wa Aman mjini Zanzibar.

Wakati huo huo; Imani Makongoro anaripoti kuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame atashindwa kushuhudia fainali ya Michuano ya klabu za Soka Afrika Mashariki na Kati 'Cecafa' Kagame Castle Cup hapo kesho.

Rais Kagame ambaye amekuwa mdhamini mkuu wa michuano hiyo tangu 2002 anatarajiwa kuwakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo wa nchi ya Rwanda, Protas Mitani kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye.

Musonye alisema walimwalika rais Kagame katika fainali hizo, lakini kutokana na sababu ambazo ziko juu ya uwezo wake hataweza kuja ila atawakilishwa na Waziri Mutani katika sherehe hizo za kufunga mashindano hayo.

ìRais Kagame hataweza kuja katika fainali za mashindano haya kutokana na kuwa na shughuli nyingine za kitaifa, lakini Mitani ambaye ni Waziri wa Michezo atamwakilisha,î alisema Musonye.

Alisema licha ya kutokuwepo katika fainali hizo rais Kagame ametoa dola 60,000 kama zawadi kwa washindi wa michunao hiyo.

Mshindi wa kwanza katika fainali hizo atajinyakulia kitita cha dola 30,000 wakati wa pili ataondoka na dola 20,000 huku wa tatu akijinyakulia dola 10,000.


Source: Mwananchi News Paper

No comments:

Post a Comment