Friday, October 5, 2012

TFF yaipiga Yanga faini Sh 3m



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeitoza Yanga faini ya shilingi milioni tatu kutokana na kosa la kutovaa jezi za wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, katika mechi mbili zilizopita dhidi ya African Lyon na Simba.

Kwa mujibu wa kanuni ya 8 ya Ligi Kuu Bara, kifungu kidogo cha 38, iwapo timu haitavaa jezi ya mdhamini, itachukuliwa hatua ya kutozwa faini ya Sh milioni 1.5.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema adhabu hiyo inatolewa kwa mujibu wa kanuni za udhamini. 
“Awali Yanga haikuvaa jezi yenye nembo ya wadhamini wakuu, Vodacom, katika mchezo wao dhidi ya African Lyon wiki iliyopita na tumewaandikia barua ya kutakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni moja na nusu.

“Pia katika mchezo wa leo (juzi) hawajavaa pia jezi hizo, kanuni zipo wazi, tutawaandikia barua nyingine ya kuwataka walipe shilingi milioni moja na nusu nyingine kutokana na kukaidi taratibu.

“Hili litakuwa fundisho kwa timu nyingine ambazo zitafanya kama walivyofanya Yanga, kwani taratibu zinaeleweka, kila timu inatakiwa ikubaliane na kile ambacho kinapangwa katika kanuni,” alisema Wambura.

Yanga imeamua kutovaa jezi za Vodacom kwa madai kwamba kuna alama ya mduara mwekundu katika jezi hizo, rangi ambayo hutumiwa na wapinzani wao, Simba.

Na Khadija Mngwai, GPL

No comments:

Post a Comment