Friday, October 12, 2012

Coastal waahidiwa 20m waichinje Simba



WADAU wa Coastal Union wa jijini Tanga, wamewaahidi wachezaji wa timu hiyo na benchi la ufundi Sh milioni 15 endapo kesho wataifunga Simba, huku uongozi ukitoa milioni tano kama kawaida kila timu hiyo inaposhinda.

Timu hizo zinatarajiwa kupambana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, kesho Jumamosi.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa wadau hao wameamua kutoa ahadi hiyo ili wachezaji wajitume na wapate ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Watu wa karibu na timu wamewaahidi milioni 15 na zinaweza kuongezeka, pia uongozi wa timu utatoa milioni tano kama kawaida kila inaposhinda,” kilisema chanzo hicho. 

Coastal imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Ghymkhana Bombo jijini humo lakini jana ilihamia kwenye Uwanja wa Mkwakwani na leo wachezaji watapasha misuli Ghymkhana kabla ya mtanange huo wa kesho. 

Naye Katibu Mkuu wa Coastal Union, El-Siagi Kassim, amesisitiza kwa kusema: “Tunajiandaa kuona tunafanya vizuri, hakuna zaidi ya ushindi.”

Tayari Simba wapo jijini Tanga ambako walifika salama juzi kwa ajili ya mechi hiyo itayokuwa ya kwanza kwao kucheza nje ya Dar es Salaam, msimu huu.

Na Lucy Mgina na Khadija Mgwai

No comments:

Post a Comment