Wednesday, August 29, 2012

YANGA KUCHEZA NA COASTAL JUMAMOSI


Mabingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (KAGAME) timu ya Young Africans Sports Club iliyokuwa imeweka kambi ya wiki moja nchini Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu, itashuka dimbani kucheza na Coastal Union ya Tanga siku ya jumamosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akiongea na mtandao wa klabu www.youngafricans.co.tz Afisa Habari wa klabu ya Yanga Louis Sendeu amesema watatumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya ligi kuu nchini, inayotazamiwa kuanza mwezi septemba.

Young Africans iliyokuwa nchini Rwanda kwa muda wa wiki moja, ilicheza michezo miwili ya kujipima nguvu na timu za Rayon Sports na Police Fc.

Katika mchezo wa kwanza, Young Africans iliifunga Rayon Sports mabao 2- 0, mabao yaliyofungwa na Saimon Msuva na Hamis Kiiza, huku mechi ya pili dhidi ya Police Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yakifungwa na Nadir Haroub 'Cannavaro' na Stephano Mwasika.

Timu ilirejea siku ya jumatatu kutoka Kigali Rwanda na jana iliendelea na mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola ambapo inaendelea na mazoezi kila siku asubuhi kwa kipindi hichi chote cha maandalizi ya ligi kuu.

Aidha mchezaji mpya kutoka APR FC ya nchini Rwanda, mlinzi Mbuyu Twite anataajiwa kuwasili kesho majira ya mchana saa 9, akitokea nchini Rwanda alipobakia kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuja nchini na familia yake.

Mbuyu Twite anawasili kesho mchana kwa shirika la ndege la Rwanda Air akiwa sambamba na mjumbe wa kamati ya utendaji Abdallah Bin Kleb aliyekua amebakia pia nchini Rwanda kuhakikisha Twite anakamilisha zoezi hilo.

Viiingilio vya mchezo dhidi ya Coastal Union siku ya jumamosi ni:
VIP A, 20,000/=
VIP B & VIP C , 10,000/=
Orange, 5,000/=
Blue & Green 3,000/=

Wapenzi, wanachama na washabiki wa Young Africans mnaombwa kujitokeza kwa wingi siku ya jumamosi Uwanja wa Taifa , itakua ni fursa ya kuwaona wachezaji wote waliosajili msimu huu.

"YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO"

No comments:

Post a Comment