Release No. 131
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Agosti 3, 2012
LIGI DARAJA LA KWANZA SASA TIMU 24
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na mabadiliko ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya mabadiliko ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na mabadiliko hayo, timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kutokana na ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Timu ya kwanza kutoka kila kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu itakayoungana na hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa timu zilizoshika nafasi ya pili katika kila kundi.
Ili kufikisha idadi ya timu 24 kwenye FDL, Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya Taifa kutoka vituo vyote vitatu vya ligi hiyo zimepanda daraja.
Sasa timu 24 za FDL ni Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar es Salaam), Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mbeya City (Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na Morani (Manyara).
Nyingine ni Moro United (Dar es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza), Polisi (Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara), Polisi (Tabora), Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es Salaam), Transit Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam)
Timu nne zitashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa kila kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo utakaohusisha mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na zisizozidi 20. Ligi za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini).
Ligi ya mkoa itashusha timu mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi za wilaya zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu zaidi ya 20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja kwa mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya wilaya.
Mabingwa wa wilaya katika mkoa husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata timu mbili zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na mabadiliko hayo ya mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya Wilaya (Ligi Daraja la Nne).
TFF inasisitiza kuwa kwa mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa madaraja yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati mmoja.
Usajili wa hatua ya kwanza ni kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha usajili ni Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja yote zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja la Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya zenyewe zitaanza Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua msimu kwa madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na makamu bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe la FA itaanzia wilayani Septemba 24 mwaka huu.
BINGWA MICHUANO YA BANCABC SUPER 8 KUPATA MIL 40/-
Bingwa wa michuano ya BancABC Super 8 inayoanza keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza na Arusha atapata sh. milioni 40 wakati makamu bingwa sh. milioni 20. Pia timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu fainali kila moja itapata sh. milioni 15 wakati zilizobaki kila moja itapata sh. milioni 5.
Timu zimepangwa katika makundi mawili ya A na B. Kundi A lina timu za Simba (mabingwa wa Tanzania Bara), Jamhuri, Zimamoto na Mtende zote za Zanzibar. Kundi ni Super Falcon (mabingwa wa Zanzibar), Azam, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro zote za Tanzania Bara.
Mechi za ufunguzi keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) ni Simba vs Jamhuri (Dar es Salaam), Zimamoto vs Mtende (Mwanza), Mtibwa Sugar vs Polisi Morogoro (Arusha) na Super Falcon vs Azam (Zanzibar). Awali mashindano yalikuwa yaanze Agosti 4 mwaka huu lakini yamesogezwa mbele kwa siku moja.
Hatua ya makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu. Mechi za nusu fainali na fainali zote zitachezwa Dar es Salaam.
Mdhamini bancABC atagharamia usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine, malazi na jezi. Yanga imejitokea kwenye mashindano hayo na nafasi yake imechukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Vodacom.
KOZI YA UONGOZI YA FIFA KUANZA AGOSTI 6
Kozi ya Uongozi na Utawala ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itafanyika Msimbazi Center jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-11 mwaka huu ikiwa na washiriki 30.
Washiriki wa kozi hiyo itakayonedeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ni viongozi kutoka TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, klabu za Ligi Kuu na viongozi wa mpira wa miguu wa wanawake.
Walioteuliwa kushiriki ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA Amani Makungu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy Kiondo, Stanley Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud Mvella.
Wengine ni Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, wenyeviti wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi), Dodoma (Nassoro Kipenzi) na Pascal Kihanga (Morogoro).
Makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent Majiri), Morogoro (Hamisi Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya) na Dodoma (Stuart Masima). Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Hilal na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.
Washiriki wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, Ofisa Habari, Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy Kabwe, Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba, Ofisa Sheria wa TFF, Neema Lucumay, Ofisa wa Mpira wa Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma (Mpira wa miguu wa wanawake) na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.
STARS KUIKABILI BOTSWANA AGOSTI 15
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Agosti 15 mwaka huu itapambana na Botswana (Zebras) katika mchezo maalumu wa Kalenda ya FIFA utakaofanyika jijini Gaborone.
Tayari Kocha Kim Poulsen alishatangaza kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Agosti 8 mwaka huu tayari kwa mechi hiyo ya kirafiki ya kujipima nguvu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment