MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga jana walitumia uzoefu wa michuano ya kimataifa kucheza nusu fainali Kombe la Kagame baada ya kuifunga Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3 kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, sasa Yanga itakumbana na APR ya Rwanda iliyokuwa ya kwanza kukata tiketi ya hatua hiyo baada ya kifunga URA mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa wa pili kwa timu hizo kwenye michuano hii, baada ya awali wavaa jezi hao za njano na kijani kushinda mabao 2-0 katika wa hatua ya makundi.
Pambano hilo lililazimika kwenda hatua ya kupigiana kiki za penalti baada dakika 90 kumalizika na sare ya kufungana bao 1-1, na Yanga kufunga penalti zote tano.
Shujaa wa Jangwani alikuwa Athumani Idd aliyefunga penalti ya mwisho baada ya awali Said Mussa wa Mafunzo kushindwa kupachika wavuni kiki yake iliyogusa kidogo mwamba wa goli na kwenda nje.
Penalti zingine za Yanga zilizokwenda kugusa kamba za Mafunzo ni kupitia kwa Said Bahanuzi, Nadir Haroub, Hamis Kiiza aliyepiga penalti nzuri iliyojaa ufundi na Haruna Nyiyonzima.
Waliofunga kwa upande Mafunzo ni Mohamed Abdulrahim, Jaku Juma na Salum Said.
Katika mchezo huo ambao kipindi cha kwanza kilishuhudia Yanga walipoteana sehemu ya kiungo, walitumia mfumo wa 5-3-2, huku Mafunzo wakitumia 4-4-2.
Viungo Athumani Idd na Haruna Niyonzima walipotea katika nusu hiyo ya kwanza na kuwapa mwanya Mafunzo kuucheza mpira walivyotaka wakitumia pasi fupi-fupi, huku Yanga wakicheza pasi ndefu.
Dakika ya 22, mwamuzi Thiery Nkurunziza wa Burundi alikataa bao la Yanga lililofungwa na Hamis Kiiza akidaiwa kutokea kabla akakwamisha wavuni mpira akimalizia krosi ya Rashid Gumbo.
Baada ya kulazimisha kona tatu mfululizo, hatimaye Mafunzo walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Ally Othman aliyeunganisha wavuni kona ya Ally Juma.
Yanga walirejea kipindi cha pili na nguvu kubwa na iliwachukua dakika moja kusawazisha bao kupitia Said Bahanuzi aliyetikisa kamba za Mafunzo kwa kichwa akimalizia krosi ya Juma Abdul.
Mshambuliaji Jerryson Tegete aliyeingia baada ya dakika 10 za kwanza, nusu ya pili ya mchezo kuchukua nafasi ya Rashid Gumbo, alishindwa kufanya matokeo kuwa 2-1 baada shuti lake kukosa shabaha akiwa ndani ya 18 katika dakika ya 63.
Kipa namba moja wa Yanga, Yaw Berko alishindwa kuendelea na mchezo katika dakika ya 70 na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Mustafa baada ya kuumia paja.
Mpira ulisimama tena katika dakika ya 80 kufuatia Juma Othman wa Mafunzo kupoteza fahamu kwa muda baada ya kugongana na mchezaji wenzake katika harakati za kuokoa hatari langoni kwake.
Kocha wa Mafunzo, Hamed Suleiman alisema ameridhika na matokeo na kwamba, kikosi chake kilicheza vizuri lakini bahati haikuwa yao.
Thomas Saintfiet alikipongeza kikosi chake kwa ushindi huo na kusema mchezo ulikuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kucheza vizuri.
Hata hivyo, Saintfiet alionyesha wazi na kukerwa na viwango duni vya baadhi ya wachezaji wake na kusema atalazimika kuwaeleza ukweli.
Saintfiet alisema kuna baadhi ya wachezaji ndani ya kikosi chake hawastahili kuendelea kuwapo na ameshangazwa na uongozi umeendelea kuwalea.
"Kuna wachezaji ni wazi hawastahili kubaki Yanga, nitapendekeza tuwatoe kwa mkopo kwenda timu nyingine na wengine watafute timu za kucheza," alisema kocha huyo mpya Yanga.
Katika mchezo uliotangulia, APR ilikuwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya kuifunga URA ya Uganda kwa mabao 2-1 katika mchezo uliojaa kila aina ya ushindani.
APR walikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika 13 kupitia kwa Iranzi Jean kabla ya Seleman Ndikumana kuongeza lingine na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa na mabao hayo.
Kipindi cha pili, URA walifunga bao pekee kupitia kwa Robert Ssentongo katika dakika ya 57 baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa APR na kufunga kwa shuti kali.
APR ililazimika kucheza pungufu dakika za mwisho baada ya mchezaji Kabange Twita kumchezea vibaya Said Kyeyune wa URA.
Sweetbert Lukonge, Mwananchi
No comments:
Post a Comment