Friday, July 6, 2012

OKWI AELEZA KILA KITU KUHUSU YANGA


MSHAMBULIAJI nyota wa Simba, Emmanuel Okwi ameitaka Yanga kuonana na viongozi wa Simba kama ina nia ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Pamoja na hivyo, Okwi amesisitiza, ndoto yake ni kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na kesho au keshokutwa ataanza safari ya kwenda nchini Italia kufanya majaribio katika klabu ya Parma.

Akizungumza jana kutokea Kampala, Uganda, Okwi alisema ameshitushwa na taarifa za yeye kujiunga na Yanga na kusisitiza kuwa anapenda kuishi maisha kwa kufuata taratibu.

“Ninaweza kucheza Yanga kwa kuwa soka ni kazi yangu, lakini bado nina mkataba na Simba. Waambie Yanga wazungumze na Simba halafu nitazungumza nao, lakini hayo yaliyoelezwa wasiyafuatilie,” alisema.

Alipoulizwa kuwa kuna baadhi ya wadau wa Yanga wakiongozwa na mtoto wa kigogo mkubwa kabisa walimfuata Kampala na kuzungumza naye jijini Kampala kwa ajili ya kufanya usajili ajiunge na Yanga, alisema: “(kicheko), hapa Kampala ninakutana na Watanzania wengi sana, wako Yanga wengine Simba. Sidhani kama ni vibaya kuzungumza na mtu, sina uadui,” alisema.

Jana, mashabiki wa Simba walikuwa katika hofu kuu kuhusiana na taarifa za Okwi kusaini kuichezea Yanga kwa ajili ya msimu ujao. Hata hivyo, mkataba wa Okwi unaomalizika Julai mwakani.

Okwi alikataa kulizungumzia suala hilo na kusisitiza anataka kumalizia suala lake la kupata Visa kwa ajili kwenda nchini Italia kwa ajili ya majaribio.

“Nafikiri nitapata leo ili nianze safari mapema, sasa niko kwenye ubalozi wa Italia, niache nishughulikie kwanza. Tunaweza kuzungumza vizuri zaidi baadaye,” alisema.

Pamoja na maelezo hayo ya Okwi, taarifa za uhakika zinaeleza Yanga imekuwa ikifanya naye mazungumzo kwa lengo la kuvunja mkataba wake na Simba kwa kitita kikubwa cha fedha.

Na Saleh Ally, GPL

No comments:

Post a Comment