Monday, July 23, 2012

Cecafa yazibadilishia ratiba Simba, Yanga


BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), limebadilisha ratiba ya Kombe la Kagame kwa kuzingatia uwepo wa klabu za Simba na Yanga.

Mpaka sasa michuano hiyo ipo katika hatua ya robo fainali, raundi ya kwanza ikitarajiwa kuanza leo kwa URA ya Uganda kuvaana na APR ya Rwanda na baadaye Mafunzo kuumana na mabingwa watetezi, Yanga huku kesho Atletico ya Burundi ikicheza na AS Vita ya DR Congo ikifuatiwa na mtanange kati ya Azam na Simba.

Ratiba inaonyesha kuwa Jumatano ni siku ya mapumziko halafu mechi zote za nusu fainali zitachezwa Alhamisi, lakini Cecafa imesema kuwa kama Yanga na Simba zitavuka hatua hiyo, Jumatano Yanga itaanza kucheza halafu kesho yake Wekundu watakuwa mzigoni lakini kama mojawapo ya timu hizo itatolewa, ratiba itabaki kama ilivyo.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alisema mabadiliko hayo yatafanywa ikiwa ni mapendekezo ya watu wa usalama ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kutokea kama timu hizo zitacheza siku moja katika mechi tofauti.

“Mabadiliko hayo yatachukua nafasi endapo timu hizo zinaweza kuvuka hatua ya robo fainali na kuingia nusu fainali. Sisi tumeona ni vyema tukakubali ushauri huo kutoka kwa watu wa usalama ambao wameona kunaweza kutokea vurugu baina ya mashabiki wa timu hizo,” alisema Musonye.

Aidha, Musonye alisema Mafunzo ambayo leo itaumana na Yanga, itamkosa mchezaji wake mmoja, Makame Haji ambaye ana kadi mbili za njano, huku akiweka wazi kwamba mpaka sasa tangu michuano hiyo ilipoanza, kuna kadi moja tu nyekundu iliyotolewa kwa kipa wa Tusker, Boniface Oluoch.

Na Khatimu Naheka

No comments:

Post a Comment