Timu za Azam FC na Yanga zimejitoa kwenye michuano maalumu ya BancABC kwa kile walichodai kuwa wanapumzisha wachezaji wao.
Hatua ya timu hizo za juu katika Ligi Kuu Bara, imekuja siku moja baada ya Simba kuweka bayana juzi kuwa hawana uhakika wa kushiriki kwa kuwa wana ratiba yao inayohusisha Simba Day.
Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alisema kuwa wachezaji wake wanatakiwa kupumzika kujipanga kwa mechi za Ligi Kuu baada ya kumalizika kwa Michuano ya Kombe la Kagame.
Naye Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa alisema kuwa ni ngumu kwao kushiriki labda wachezaji wang’ang’anie lakini itawaumiza sana.
Wachezaji waliozungumzia suala hilo kwa masharti ya kutotajwa majina yao kukwepa kuingilia uhuru wa viongozi, walisema kwamba tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Aprili mwaka huu hawajapmzika, hivyo wanataka kupumzika japo kwa siku chache kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya.
ìLigi imeisha tumengia kwenye kambi ya timu ya taifa, tumecheza na Ivory Coast, tumecheza na Gambia, tumecheza na Msumbiji na baada ya hapo tumerudi hapa, tunaingia kwenye Kombe la Urafiki na tukaingia moja kwa moja kwenye Kombe la Kagame, jamani tena tutoke hapa tuingie kwenye mashindano mengine, hatuwezi labda tucheze kama adhabu,” walisema.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa hawajapata barua rasmi za kujitoa kwa timu hizo wakipata ndiyo watajua cha kufanya.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar, (ZFA), Masudi Attai, alisema kuwa wamepokea kwa mikono miwili mwaliko wa kushiriki kwenye Kombe la BancABC Supa 8.
Kauli ya Attai imekuja kufuatia kuanzishwa kwa michuano yenye lengo la kufanya maandalizi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ambayo inatarajia kuanza Agosti 4 hadi 18, ikishirikisha timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara.
Alisema siku za nyuma kulikuwa na Kombe la Muungano ambalo lilikuwa likizifanya pande hizi mbili kukutana kila mwaka na kubadilishana uzoefu lakini lilifutwa, sasa kupitia michuano hii hilo litawezekana.
- Kandanda (Galacha)
No comments:
Post a Comment