MSANII wa filamu Bongo aliyekuwa ameenda kupata matibabu katika Hospitali ya Saifee iliyopo jijini Mumbai, India, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ amepata nafuu na kwa sasa anaendelea na dozi ili aweze kupona kabisa.
Akizungumza na Risasi Jumatano juzi nyumbani kwao Tabata jijini Dar, msanii huyo alisema sasa hivi afya yake imeimarika tofauti na alivyokuwa awali hivyo anawashukuru wote waliomsaidia na kwamba yeye hana cha kuwalipa ila Mungu atawalipa.
“Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwani hali yangu inaendelea vizuri, kinachonisumbua ni ukali wa hizi dawa tu kwani kuna wakati mwingine nakosa nguvu lakini madaktari waliniambia nizitumie mpaka zitakapoisha,” alisema Sajuki na kuongeza:
“Pia niwashukuru Watanzania kwa michango yao, hakika wameonesha ubinadamu wa hali ya juu kwangu lakini nikanushe taarifa za kwamba nimerejea kama nilivyokwenda, kwa aliyeniona wakati naondoka atakubaliana na mimi kuwa afya yangu imetengemaa kwa kiasi flani.”
Mbali na shukrani kwa Watanzania, Sajuki aliwashukuru pia madaktari wa hospitali ya Saifee kwa uangalizi waliompatia ikiwemo kumpa chakula kizuri kilichokuwa kikihitajika kutokana na dawa anazotumia.
“Nawashukuru sana wale madaktari kwani wamenitibu chini ya uangalizi mzuri kiasi cha kunifanya nipate nafuu hii,” alisema.
Sajuki alianza kusumbuliwa na uvimbe mwaka jana ulioanzia mkononi kisha ndani ya mwili kwenye ini na baadae ikagundulika kuwa, siyo kwenye ini tu bali umesambaa hadi sehemu nyingine za tumboni.
Risasi Jumatano linamuombea kwa Mungu Sajuki apone kabisa, apate nguvu za kumuwezesha kurejea katika ulingo wa filamu ili aendelee kutuelimisha na kutuburudisha tunapokuwa tumejipumzisha majumbani mwetu.
Imeandikwa na Musa Mateja, Imelda Mtema na George Kayala.
Na Waandishi, GPL
No comments:
Post a Comment