Friday, June 22, 2012

Kikwete awapa mtihani viongozi wa kikapu


RAIS Jakaya Kikwete ameutaka uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, TBF, kuhakikisha timu inatwaa ubingwa wa Kikapu Kanda ya Tano Afrika na kuweka msingi mzuri kwa Michezo ya Olimpiki ya 2016.

Kikwete aliyasema hayo juzi alipokutana na uongozi wa shirikisho hilo Ikulu, jijini Dar es Salaam lengo likiwa kuangalia maendeleo ya mchezo huo nchini. Kabla ya kuwa Rais, Kikwete alikuwa mlezi wa mchezo huo.

Hatua hiyo ya Kikwete kukutana na viongozi hao ni siku moja baada kukutana na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania, RT, kufahamu matatizo yao.

Katika mazungumzo hayo, Rais aliwataka TBF kuyatumia makampuni ya Coca-Cola, bia(TBL) na wengine na kusema naye atatia msukumo wa makampuni kusaidia kuendeleza mchezo huo.

"Nitakuwa mstari wa mbele kusaidia mpira wa kikapu, shabaha yangu ni kuona eneo hili nalo linapiga hatua katika kikapu na naamini majawabu yake yatapatikana lakini naamini hayo kama mtakuwa na mipango madhubuti kuendeelza mchezo huo...," alisema.

Mbali na hayo, TBF iliwasilisha ombi kwa Serikali kutoa kipaumbele katika awamu ya pili ya ujenzi wa Uwanja wa Taifa kwa kujenga uwanja mkubwa michezo wa ndani pamoja na serikali kusaidia kupatikana kocha wa kikapu kutoka nje.

Kikwete aliishukuru TBF, Kocha Greg , timu ya New York Knicks ya Marekani, Chuo Kikuu Cha Wake Forest cha Marekani na Coca-Cola kwa vifaa walivyompatia kama sehemu ya hamasa ya mchezo huo.

"Nikiwa katika safari zangu na nitakapokwenda Marekani nitajitahidi kuwasiliana na timu ya New York Knicks na wadau wengine kuwaomba waendelee kushirikana katika maendeleo ya mchezo wa kikapu nchini.

Katika mkutano huo, timu ya New York Kniks ilimpa jezi na jaketi kwa niaba ya kocha Greg Brittenham wa timu hiyo inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Wake Forest ambako Brittenham ni mkurugenzi wake wa Michezo.

Brown Msyani, Mwananchi

No comments:

Post a Comment