Thursday, June 21, 2012

Juma Mgunda kocha mpya Coastal

UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umemteua Juma Mgunda kuwa kocha mkuu baada ya Jamhuri Kiwehlo ‘Julio’ kubanwa na shuguli zake binafsi ikiwamo kuwa nje ya nchi mara kwa mara.

Akizungumza na Mwananchi, msemaji wa timu hiyo Edward ‘Edo’ Kumwembe alisema uongozi wake umeamua kumpa ukocha mkuu Mgunda baada ya mipango yao ya kumnyakua kocha wa Bandari ya Mombasa Rashid Sheduu kukwama.

“Tulifanya mazungumzo na Sheduu na alikuwa ameshakubali kuinoa timu yetu, lakini kabla hatujaingia naye mkataba timu yake ya Bandari ikamuongezea, hivyo madaraka yote ya ukocha sasa tumeyakabidhi kwa Mgunda,"alisema Kumwembe.

Awali Mgunda alikuwa kocha msaidizi wa timu hiyo huku Julio akiwa kocha mkuu, lakini kocha Julio mwenye maneno mengi aliondoka mzunguko wa pili msimu uliopita na kwenda kusaka timu nchini Oman ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto wake kusaka soka la kulipwa nchini humo.

Kumwembe alisema kuwa Mgunda atasaidiwa na aliyekuwa kocha wa timu ya Villa Squad, Habibu Kondo.

Alisema kikosi cha Coastal kitaanza rasmi mazoezi mapema wiki ijayo kikiwa na wachezaji wake wapya ambao ni Razak Khalfan (African Lyon), Othman Omary (Oljoro JKT), Atupele Green (Yanga B), Jackson Chove (JKT), Juma Mpongo (Kiyovu ya Rwanda), Nsa Job, Sudi Mohamed (Toto), Seleman Selembe (Azam).

Sosthenes Nyoni

No comments:

Post a Comment