Friday, May 4, 2012

WEMA ANASWA AKISOMEWA DUA


IKIWA ni siku chache baada ya mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’ atangaze rasmi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamitindo Jokate Mwegelo, aliyekuwa mpenzi wa msanii huyo, Wema Isaac Sepetu, Jumapili iliyopita alinaswa akisomewa dua na watoto yatima.
Wema alisomewa dua hiyo na watoto wa Kituo cha Kulelea Yatima cha Chakuwa kilichopo Sinza Mori, jijini Dar es Salaam huku zoezi zima likiongozwa na maustaadhi.

Staa huyo alikwenda kituoni hapo kwa lengo la kutoa sadaka kwa watoto hao ili kutimiza maagizo ya Mungu ya kutaka wasiojiweza wasaidiwe na wanaojiweza.

AKALISHWA CHINI
Mara baada ya kukabidhi sadaka yake ambayo ilikuwa juzuu, juisi na biskuti ndipo watoto hao walimkalisha staa huyo kwenye mkeka na kumwangushia kisomo cha nguvu wakiinua mikono juu huku wakimzunguka kwa mizunguko kumi.

MAJINA 99 YA MUNGU YATAJWA
Aidha, sala ya watoto hao wake kwa waume iliambatana na kutaja majina 99 ya Mungu huku Wema akiitikia amina na yeye mikono akiiweka kwa ishara ya maombi.

Wema siku hiyo alivaa gauni maarufu kwa jina la dila, kichwani alitupia khanga ili kuziba nywele ingawa ziliendelea kuonekana sehemu chache.
Kwa mujibu wa imani ya Kiislam, mwanamke anapokuwa anaswali anatakiwa kufunika kichwa chote ili kuruhusu malaika wa Mungu kumkaribia.

YATIMA AZUNGUMZA NA PAPARAZI
Yatima mmoja ambaye hakuwa tayari kujitambulisha jina, aliulizwa na mwandishi wetu kama yeye na wenzake wanakijua walichokuwa wanakifanya.

“Tulikuwa tunamsomea kisomo dada Wema. Mungu atamsaidia, atamlinda atamuondolea na nuksi, mabalaa na kila shari. Sisi huwa tunafundishwa kuwa ukiomba kwa Mungu kwa dhati hachelewi kukujibu,” alisema mtoto huyo.

KINYWANI KWA WEMA
Baada ya dua hiyo, paparazi wetu alimuuliza Wema kisa cha kuamua kupeleka sadaka kwa watoto hao ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Unajua unaweza ukatumia fedha nyingi kila siku lakini ukusahau kitu cha muhimu ambacho Mungu alikiagiza, kujumuika na watoto yatima kama hawa.

“Mimi nawapenda sana watoto hawa. Nimefurahi sana kuniombea kwani maombi yao yanafika haraka kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Wema.

KUONDOA NUKSI
Aidha, Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006 aliweka wazi kwamba anaamini maombi ya watoto hao yatamwondolea mikosi, nuksi na matukio yote mabaya kwa kuwa Mungu atamshushia malaika wa kumlinda.

HISTORIA YA WEMA
Msanii huyo ndiye supa staa anayeongoza kwa matukio makubwa, mazito yenye ujazo wa kiskendo ndani yake tangu aliponyakua taji la Miss Tanzania.

Mara nyingi mwenyewe amekuwa akidai kukerwa na skendo hizo wakati mwingine akiwatupia madongo mapaparazi kwamba wamekuwa wakimzushia ingawa baadaye hugundulika hakuna uongo.


Na Imelda Mtema, GPL

No comments:

Post a Comment