Monday, May 28, 2012


TIMU ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, imekubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wao, Ethiopia katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa uliopo katika Jiji la Addis Ababa.

Mchezo huo ulikuwa ni wa hatua ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC).

Kabla ya kwenda Ethiopia, Twiga haikuonyesha dalili nzuri baada ya kukubali vipigo vikali vya jumla ya mabao tisa katika michezo miwili ya kirafiki.

Awali, timu hiyo ilifungwa na Zimbabwe mabao 4-1 kabla ya kukubali kipigo cha mabao 5-3 kutoka kwa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Banyana Banyana, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Bao pekee la Twiga katika mchezo wa jana, lilifungwa katika kipindi cha kwanza na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Fatma Mustafa.

Twiga inatarajia kurejea nchini leo kuendelea na maandalizi ya mchezo wa pili dhidi ya timu hiyo utakaopigwa Juni 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kama kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Charles Boniface Mkwasa, kinataka nafasi ya kushiriki michuano hiyo itakayofanyika Novemba, mwaka huu nchini Guinea ya Ikweta, itabidi kipate ushindi wa bao moja au zaidi katika mchezo huo wa nyumbani.

Na Khatimu Naheka

No comments:

Post a Comment