KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeipa madaraka sekretarieti ya Klabu ya Yanga iliyo chini ya Katibu Mkuu wa timu hiyo, Selestine Mwesigwa, kushikilia madaraka kwa muda, mpaka hapo uamuzi mwingine utakapofanyika.
Uamuzi huo kutoka kwa kamati hiyo, unakuja kufuatia mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, kujiuzulu nafasi hiyo huku wajumbe kumi nao wakifanya uamuzi kama huo, hali iliyozua sintofahamu ndani ya timu hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema kamati yake iliyoketi Mei 26, mwaka huu, imetoa mwongozo huo kutokana na Kamati ya Utendaji ya Yanga kutotimiza idadi ya angalau asilimia 50 ya wajumbe kutokana na wengi wao kujiuzulu.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji ya Yanga haikuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa ibara ya 32, kifungu kidogo cha kwanza ndani ya katiba ya klabu hiyo.
Mgongolwa aliendelea kusema kuwa wajumbe pekee wa kamati hiyo ya utendaji waliosalia ni wane ambao ni Sarah Ramadhan, Titos Osoro, Mohamed Bhinda na Salum Rupia wakati walipaswa kuwa angalau saba.
“Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilikutana Mei 26, mwaka huu kutoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya Yanga baada ya wajumbe wake kadhaa kujiuzulu na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilikuwa imeomba mwongozo huo wa TFF,” alisema Mgongolwa.
“Kwa sasa shughuli za kila siku za klabu hiyo zitaendelea kufanywa na sekretarieti ya Yanga ambayo kiongozi wake ni katibu mkuu.”
Na Khatimu Naheka
No comments:
Post a Comment