Monday, May 14, 2012

Papic: Nchunga akiondoka nitarudi Yanga


SIKU chache baada ya uongozi wa Yanga kutangaza rasmi kumtema kocha wao Kosta Papic, Mserbia huyo ameibuka na kusema anaweza kurejea Jangwani ikiwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, ataondoka madarakani.

Papic ambaye alishindwa kuiongoza klabu hiyo katika michezo minne ya mwisho ya ligi kuu kutokana na kuisha kwa kibali chake cha kufanya kazi nchini, kwa muda mrefu amekuwa akikwaruzana na uongozi wa klabu hiyo kwa kile alichokiita kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Papic alisema amesikitishwa na klabu hiyo kushindwa kulitetea taji lake la ubingwa, hivyo ataangalia uwezekano wa kurudi kukifundisha kikosi hicho endapo tu Lloyd Nchunga na uongozi wake, utaondolewa katika madaraka.

Papic alisema uongozi wa Nchunga umechangia kwa kiasi kikubwa klabu hiyo kumaliza vibaya hasa kutokana na kushindwa kuonyesha uwajibikaji ipasavyo katika nyanja mbalimbali za uongozi, hali iliyosababisha timu ishindwe kupata maandalizi mazuri kabla ya mechi mbalimbali za ligi hiyo.

“Nimesikia taarifa za Lloyd (Nchunga) kwamba amesema hatanipa mkataba mwingine ingawa mimi bado hajaniambia rasmi, lakini kuhusu suala la mimi kurudi Yanga linawezekana iwapo tu yeye (Nchunga) na uongozi wake wataondoka madarakani na kuja viongozi wengine kabisa,” alisema Papic, mwenye umri wa miaka 56.

“Yanga kupoteza taji kwa asilimia kubwa amesababisha yeye (Nchunga) na siku zote uongozi wake umekuwa ukishindwa kutoa maandalizi mazuri kwa timu ili iweze kufanya vizuri jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa Yanga kumaliza ikiwa katika nafasi ya tatu,” aliongeza Mserbia huyo.

Na Khatimu Naheka

No comments:

Post a Comment