Saturday, May 12, 2012

Maajabu msanii wa ubakaji


KITENDO cha msanii Muhogo Soud Jumapili kudaiwa kumbaka msichana ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE) cha jijini Dar (jina linahifadhiwa) kimeongeza maajabu katika tasnia ya filamu hapa nchini, Risasi Jumamosi limebaini.

Maajabu hayo yamekuja baada ya Muhogo kushiriki katika filamu ya Kijiji cha Tambua Haki sambamba na wasanii wengine waliopata matatizo hivi karibuni, Steven Charles Kanumba na Kajala Masanja.

Msanii huyo anaonekana katika kava la filamu hiyo akiwa amepigwa kabali na staa aliyetangulia mbele ya haki, Kanumba huku Kajala ambaye yuko katika Gereza la Segerea, jijini Dar kwa tuhuma za kutakatisha fedha haramu akiwa amepozi nyuma yao.

“Haya ni maajabu, wote walionekana katika kava lile wamepatwa na matatizo makubwa,” alisema mmoja wa wasanii ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini.

Kwa mujibu wa shuhuda wetu, Mei 5, mwaka huu, Muhogo ambaye anafanya kazi za sanaa katika Kikundi cha Tanganyika cha Kinondoni jijini Dar alidaiwa kumrubuni msichana huyo kwa kumwambia kuwa angemfanyia mipango ya ‘kushuti’ katika filamu mpya ya msanii Single Mtambalike ‘Richie’.

Muhogo alimwita msichana huyo nyumbani kwake, Ilala jijini Dar kisha kumlazimisha kufanya naye mapenzi bila ya ridhaa yake.

“Baada ya msichana yule kufika kwa Muhogo kwa lengo la kupelekwa kwa Richie, msanii huyo alifunga mlango na kumtaka kimapenzi na alipokataliwa ndipo alipotumia nguvu,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kimesema kuwa Muhogo alidaiwa kumbaka msichana huyo sambamba na kumwingilia kinyume na maumbile baada ya kumchania nguo yake ya ndani.

Baada ya msanii huyo kumaliza haja zake, msichana huyo alikwenda kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Urafiki, Manzese jijini Dar na kupewa hati ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar.

“Baada ya kurudi nyumbani kwake, hali yake haikuwa nzuri ikabidi kesho yake arudi tena hospitalini hapo na kulazwa kwa siku mbili,” kisema chanzo hicho.

Hata hivyo, askari wa Kituo cha Urafiki walimshauri msichana huyo kufungua mashtaka katika Kituo cha Polisi cha Pangani Ilala ambako alipewa RB namba ILA/RB/1763/2012 KUBAKA.

Mei 10, mwaka huu, Muhogo alipandishwa katika Mahakama ya Ilala na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Joyce Minde na kushtakiwa kwa makosa mawili ya kubaka na kumwingilia msichana huyo kinyume na maumbile. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 24, mwaka huu.

Habari imeandikwa na Issa Mnally, Erick Evarist na Gladness Mallya.

No comments:

Post a Comment